Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Tanzia : MENEJA MIPANGO NA FEDHA KAMPUNI YA MATI SUPER BRANDS LTD AFARIKI DUNIA

Goodluck Didas Silayo enzi za uhai wake 
Kampuni ya MATI Super Brands Limited imekumbwa na msiba mkubwa baada ya kuondokewa na Meneja wake wa Mipango na Fedha, Bwana Goodluck Didas Silayo, aliyefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MATI Super Brands Limited, Bwana David Damian Mulokozi, marehemu Silayo alifariki dunia usiku wa Juni 12, 2026, majira ya saa 2:00 usiku katika eneo la Chenene mkoani Dodoma, baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana na lori la semitrailer.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kutokana na ukali wa ajali hiyo, marehemu alifariki dunia papo hapo katika eneo la tukio.

Uongozi wa kampuni umesema kuwa marehemu Goodluck Didas Silayo alikuwa mmoja wa watumishi muhimu waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji na mafanikio ya kampuni hiyo kupitia weledi wake, uadilifu, bidii na uwezo mkubwa wa kupanga na kusimamia masuala ya kifedha.

“Marehemu alikuwa mtumishi mwaminifu, mchapakazi na mwenye maono makubwa. Mchango wake katika maendeleo ya kampuni yetu utaendelea kukumbukwa daima,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kifo chake kimeelezwa kuwa ni pigo kubwa si kwa familia yake pekee, bali pia kwa MATI Super Brands Limited, wafanyakazi wenzake na wadau mbalimbali waliokuwa wakifanya kazi naye.Ndg. David Mulokozi Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya vinywaji changamshi ya MATI Super brand LTD

Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa MATI Group of Companies, uongozi wa kampuni umetoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo.

Katika ujumbe wake wa faraja, kampuni imenukuu maandiko matakatifu kutoka kitabu cha Ayubu 1:21 yanayosema:

“Bwana alitoa, Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe.”

MATI Super Brands Limited imeungana na familia na wapendwa wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, huku ikiomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu Goodluck Didas Silayo mahali pema peponi na kuwapa nguvu, faraja na uvumilivu wote wanaoendelea kuomboleza msiba huo.

Chama cha waandishi wa Habari vijijini RUJAT kimetangaza kuungana na kampuni ya MATI na kinatoa salaam za rambirambi kwa Mkurugenzi wa MATI, wafanyakazi, ndugu wa Marehemu Silayo na marafiki wote.

Akitoa salaam za rambi rambi Katibu wa RUJAT Prosper Kwigize amemtaja marehemu Silayo kwamba alikuwa kiungo mhimu kati ya kampuni hiyo, wadau, wateja na vyombo vya habari katika kuiendeleza kampuni ya MATI ambayo pia ni mdau wa vyombo vya habari nchini.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana Lihimidiwe, Amina

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com