Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Abwao, alifariki dunia Jumamosi, Juni 20, 2026, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa akiendelea na matibabu.Na Lilian Kasenene, Morogoro
Wakazi wa Manispaa ya Morogoro wamejitokeza kuaga kwa mara ya mwisho mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao, nyumbani kwake eneo la Mji Mwema, Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro.
Hisia za wengi zimeonekana wazi wakati Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, alipokuwa akitoa salamu zake na kushindwa kuendelea kuzungumza kutokana na majonzi yaliyomkumba akimkumbuka rafiki na ndugu yake huyo.
Londo alisema walifahamiana na SACP Abwao tangu waliposoma pamoja katika Shule ya Sekondari Kigurunyembe mkoani Morogoro, ambapo marehemu alikuwa akimtangulia darasa moja na alikuwa mmoja wa wanafunzi waliopendwa kutokana na nidhamu na ushirikiano wake.
"Mama zetu waliishi jirani eneo la Misufini Morogoro. Hata alipoingia Jeshi la Polisi hakuwahi kubadilika, aliendelea kuwajali watu wote aliowafahamu," amesema Londo huku akibubujikwa machozi.

Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Paroko wa Parokia ya Josephine Bakhita, Padre Samuel Kasawala, waumini wamekumbushwa umuhimu wa kuishi maisha ya kumtegemea Mungu.
Padre Kasawala alisema kifo ni fumbo ambalo halichagui mtu na kwamba kila mmoja anatakiwa kuwa tayari wakati wote.
Akisoma wasifu wa marehemu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, alisema marehemu alitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka mingi katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo OCD Rorya, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simiyu na baadaye Tabora.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, SACP Mtatiro Kitinkwi, alisema Abwao alikuwa kiongozi aliyesimamia haki, nidhamu na uadilifu katika utendaji wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amesema Jeshi la Polisi limepoteza kiongozi aliyekuwa mfano wa kuigwa kwa askari na maafisa wengi nchini.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia, Thomas Abwao aliwashukuru watu wote waliochangia matibabu na kuendelea kuwa karibu na familia katika kipindi chote cha ugonjwa na msiba huo.
Baada ya ibada hiyo, mwili wa marehemu uliondoka mkoani Morogoro kuelekea Tabora kwa shughuli za kuagwa rasmi kabla ya kupelekwa Shirati wilayani Rorya mkoani Mara kwa maziko yatakayofanyika Ijumaa, Juni 26.

Social Plugin