Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema kuwa sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania ina fursa kubwa na zenye mvuto kwa uwekezaji, hivyo kuwahimiza wadau mbalimbali wa sekta hiyo kuchangamkia fursa zilizopo.
Mhandisi Sangweni amesema hayo Mei 14, 2026 jijini London, Uingereza, wakati akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini kwenye Kongamano la Nishati Afrika.
Akiwasilisha mada hiyo, Sangweni alibainisha kuwa miongoni mwa fursa zilizopo ni uwekezaji katika vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia vilivyowazi, ambapo alieleza kuwa maandalizi muhimu kuelekea mnada wa vitalu hivyo yamekamilika.
“Kinachosubiriwa kwa sasa ni kuidhinishwa kwa Mkataba Kifani wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato wa Mafuta na Gesi Asilia (Model Production Sharing Agreement – MPSA). Mara baada ya kuidhinishwa kwa MPSA hiyo, mchakato wa mnada wa vitalu utaanza mara moja,” alisema Sangweni.
Aidha, alieleza kuwa data mbalimbali za vitalu vilivyowazi zinapatikana kwa ajili ya wawekezaji kuziona na kuzinunua kwa madhumuni ya tathmini na uwekezaji. Miongoni mwa data hizo ni pamoja na data za nguvu sumaku ya miamba (magnetic), uzito wa miamba (gravity), mitetemo ya 2D na 3D pamoja na taarifa za visima.
Sambamba na hilo, Sangweni alisema kuwa ipo fursa kwa wawekezaji kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kuendeleza vitalu vya Lindi–Mtwara, Eyasi-Wembere, Mnazi Bay Kaskazini na Songo Songo Magharibi, ambavyo TPDC imeendelea kuvifanyia shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia.
Aliongeza kuwa utekelezaji unaoendelea wa miradi mbalimbali katika mkondo wa juu wa petroli, ikiwemo mradi wa uchimbaji wa visima vya uzalishaji wa gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara, umeendelea kuongeza imani kwa wawekezaji na wadau wa sekta hiyo kuwekeza nchini Tanzania.
“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, jambo ambalo limeendelea kuongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia,” alisema Sangweni.







Social Plugin