Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAHITIMU VETA SHINYANGA WATAKIWA KUTUMIA UJUZI, KUJIAJIRI BADALA YA KUSUBIRI AJIRA ZA SERIKALI

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Maganya , amewataka vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi VETA kuacha tabia ya kuilaumu Serikali kwa ukosefu wa ajira na badala yake kutumia ujuzi walioupata kujiajiri ili kukuza uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika mahafali ya chuo cha VETA Shinyanga amesema vijana wengi wamepata fursa muhimu ya mafunzo ya ufundi ambayo inapaswa kuwa mwanzo wa kujitegemea badala ya kusubiri kuajiriwa na Serikali au sekta binafsi.

Amesema vijana wanapaswa kuthamini taaluma waliyoipata kwa kuitumia katika shughuli za uzalishaji na ubunifu zitakazowawezesha kujipatia kipato pamoja na kuajiri wengine.

“Mmepata ujuzi mzuri, uutumieni vizuri. Msiende kukaa mkisubiri ajira kwa sababu mtakuwa hamjaitendea haki taaluma yenu. Nimeona mambo makubwa mnayofanya hapa chuoni, hivyo msikubali ujuzi wenu upotee,” alisema Fadhili.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuviimarisha vyuo vya VETA nchini ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kupata elimu ya ufundi stadi inayowawezesha kujitegemea kiuchumi.

Alisema vijana wanaojiunga na vyuo hivyo hawapotezi muda bali wanajenga maisha yao ya baadaye na kuandaa msingi imara wa kujikwamua kiuchumi.

Fadhili pia amewataka vijana wengine kutumia nafasi zilizopo kwenda kujifunza ujuzi mbalimbali huku akitoa rai kwa wazazi kuwapeleka watoto wao katika vyuo vya ufundi ili waweze kupata maarifa yatakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Kuhusu changamoto zinazoikabili VETA Shinyanga, amesema matatizo yaliyopo yatafanyiwa kazi na kuahidi kuyawasilisha serikalini kwa hatua zaidi.
                                                                                    
                                            Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Mbuguni, amesema chuo hicho kinaendelea kuvutia wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na ubora wa mafunzo yanayotolewa.

Amesema baadhi ya vijana kutoka nchi jirani wamekuwa wakifika katika chuo hicho kwa ajili ya kupata ujuzi wa fani mbalimbali.

Mbuguni ameiomba Serikali kuendelea kutatua changamoto zinazoikabili taasisi hiyo ikiwemo ukosefu wa uzio, uchakavu wa mitambo ya kufundishia pamoja na upungufu wa magari ya kujifunzia.

Aidha amesema jumla ya vijana 107 wamehitimu mafunzo katika fani mbalimbali.

 

 Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, amewahimiza vijana kutumia ujuzi wao kujiajiri badala ya kutegemea ajira rasmi ambazo amesema ni chache.

Amesema elimu ya ufundi stadi ina mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la ajira kwa kuwa inawapa vijana uwezo wa kuanzisha shughuli zao binafsi kwa muda mfupi.

“Ujuzi unalipa na unaweza kutoa ajira nyingi kwa haraka, hivyo vijana tumieni vizuri nafasi mlizopata,” alisema Mtatiro.

                                                                           


 



                Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro








 Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Mbuguni,








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com