Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WA SIASA WATAKA MARIDHIANO KUNUSURU NCHI

Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo ya Uma (Chauma) na aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2025, Salum Mwalimu, ametoa wito wa kuwepo kwa klasi katika kupatikana kwa maridhiano yanahitajika kwa dharura na kuonya kuwa mtu yeyote mwenye nia ya kutaka yaliyotokea Oktoba 29 yajirudie hatakuwa miongoni mwa Watanzania na anapaswa kukataliwa. 

Mwalimu ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa mjadala wa kitaifa kuhusu hatima ya nchi ulioandaliwa na Chama cha ACT Wazalendo. 

.Mwalimu alieleza kuwa kila mtu anajua kilichotokea siku hiyo ya uchaguzi, ikiwemo mauaji na uwepo wa changamoto kubwa ya ajira kwa vijana, lakini akasisitiza kuwa kikwazo kikubwa kwa sasa imekuwa ni wanasiasa kushindana maneno majukwaani na kuonyesha umahiri wa kusema badala ya kugusa kiini cha tatizo na kutoa majawabu ya kuivusha nchi.

Kutokana na hali hiyo, Salum Mwalimu alimpongeza Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kwa kuitisha mjadala huo na kumtaka asione aibu kusimamia jawabu aliloliwasilisha kupitia kijitabu chake kilichosisitiza haja ya kuanzisha jukwaa la majadiliano ya kitaifa yatakayoongozwa na misingi ya ukweli, haki na uwajibikaji. 

Mwalimu alimshauri Othman kuchukua uongozi na kuunda kamati itakayojumuisha watu mbalimbali ili kuanzisha jukwaa hilo, si kama mwenyekiti wa chama bali kama kiongozi mwandamizi wa kisiasa atakayeungwa mkono na vyama vingine, kwa lengo la kupata ukweli na kuweka mifumo ya jinsi viongozi wa kisiasa wanavyopaswa kuwajibika.

Kwa upande wake, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya siasa, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa nchi inahitaji utashi wa kisiasa kabla ya kuanza kuzungumza ukweli, huku akionya kuwa viongozi wengi wa sasa wanaonekana kuwa wepesi kukimbilia mitandao ya kijamii badala ya kuonyesha uongozi thabiti. 

Kamwaga alifafanua kuwa kiongozi mzuri ni yule anayesimama mbele na kuwa tayari kupokea lawama au kuzomewa, lakini anakaa nyuma wakati wa kupokea sifa, sifa ambayo kwa sasa inaonekana kupotea miongoni mwa viongozi.

Naye mwanasiasa Odero Odero aliwataka viongozi wa upinzani kuacha kulia na badala yake watafute suluhu ya kweli kwa kukabiliana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye meza ya mazungumzo. 

Odero aliwashauri viongozi hao akiwemo Othman Masoud, Zitto Kabwe, na John Heche kuondoa tabia ya kuogopana na kujificha kwani Rais Samia ni kama dada na mama yao, na njia pekee ya kuifikisha nchi mbali ni kukaa naye meza moja ili kieleweke. 

Suala hili la maridhiano ni sehemu ya falsafa ya uongozi ya Rais Samia kupitia '4R' zake ambazo ni Maridhiano, Ustahmilivu, Mabadiliko na Kujenga upya, ambapo hivi karibuni aliahidi kuunda kamati ya maridhiano baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com