Katika dunia ya sasa inayokabiliwa na mabadiliko ya haraka, amani imebaki kuwa nguzo kuu ya maendeleo na ustawi wa jamii ambapo hakuna taifa linaloweza kupiga hatua bila utulivu.
Amani ni hazina adimu inayotokana na juhudi na mshikamano wa watu wote, na katika hili, vijana wana nafasi ya kipekee kama nguvu kazi na warithi wa kesho.
Katika kongamano la vijana lililofanyika Wilaya ya Kibiti, mwezeshaji wa amani na utawala bora, Uzima Justin, amesisitiza kuwa ni lazima kila kijana awe mzalendo kwa kuipenda nchi yake na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuvunja amani tuliyoijenga kwa miaka 62 tangu enzi za Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Kambarage Nyerere.
Justin amewahimiza vijana kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, akifananisha majukwaa hayo na vumbi ambalo likitumiwa vibaya linaweza kuharibu kila kitu kwa kusambaza chuki na taarifa potofu.
Amesema kuwa nchi inajengwa na wazalendo na si wachafuzi, hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa za kidijitali kwa busara ili kulinda nyumba ya amani ya Tanzania.
Aliongeza kuwa hakuna sehemu nyingine ya kwenda amani ikipotea, hivyo kila mmoja anapaswa kupigania misingi ya nchi kwa udi na uvumba kwa sababu yeyote atakayejaribu kuivunja atavunjika yeye mwenyewe.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo, amebainisha kuwa takribani asilimia 67 ya nguvu kazi katika wilaya hiyo inatokana na vijana waliojikita katika sekta za kilimo, uvuvi, na ujasiriamali.
Kwa sababu hiyo, vijana ni nguzo muhimu ya uchumi inayopaswa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za nchi ili kudumisha utulivu.
Serikali kupitia uongozi wake imeahidi kuendelea kusikiliza changamoto za vijana na kuwapatia fursa za kiuchumi na mikopo, huku ikimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mkazo katika maendeleo ya kundi hilo muhimu kupitia wizara maalum.
Naye Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Amina Ali, amekumbusha kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kulinda amani ili taifa lijengeke kupitia uvumilivu.
Washiriki wa kongamano hilo, wakiongozwa na Juma Ramadhan, wameeleza kuwa ili vijana wawe mabalozi wazuri wa amani, wanahitaji kushirikishwa kikamilifu kwenye maamuzi yanayohusu mustakabali wa nchi yao.
Wamesisitiza kuwa elimu ya maadili, ajira, na fursa za biashara ni silaha muhimu zitakazowazuia vijana kukata tamaa na kujiingiza katika vitendo vya vurugu.
Social Plugin