Asema Serikali inalenga kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa kutoka njeAisisitiza Afrika kuongeza thamani ya malighafi na kuimarisha uhamishaji wa teknolojia
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania imeweka kipaumbele katika uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini ili kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.
Dkt. Mwigulu amesema hayo jijini Nairobi, Kenya alipokutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Christophe Lecourtier, kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward Summit).
“Tunaagiza kiasi kikubwa cha dawa kutoka nje ya nchi, lakini sasa tumeweka kipaumbele kuona jinsi tunavyoweza kuwekeza kwenye viwanda vya dawa ili tuzalishe hapa nchini,” amesema Dkt. Nchemba.
“Kupitia ofisi yako pamoja na wadau wengine, wanaweza kutumia fursa hii kubwa iliyopo kuja kuwekeza kwenye eneo hilo. Na kama unavyofahamu, kuwekeza Tanzania ni kuingia katika lango la ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).”
Aidha, Dkt. Mwigulu amepongeza dhamira ya AFD ya kuusaidia Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili, akieleza kuwa mradi huo ni wa kimkakati katika kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, nishati, kilimo hususan umwagiliaji pamoja na sekta ya afya kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameishukuru AFD kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
“Tunathibitisha tena dhamira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa karibu na AFD kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wetu,” amesema.
Akizungumza katika mjadala kuhusu maendeleo ya sekta ya kilimo, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuoanisha malengo ya Bara la Afrika ili kuchochea maendeleo endelevu.
“Tumekaa muda mrefu tukizungumzia kujenga uwezo badala ya kujenga miundombinu itakayowezesha bara letu na nchi zetu kuendesha ajenda zao ipasavyo,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika uhamishaji wa teknolojia na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kilimo.
“Tunatarajia ushirikiano katika uhamishaji wa teknolojia ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa matumizi ya zana za kisasa za kilimo, utekelezaji wa huduma za ugani na mifumo ya kidijitali. Si muda sasa wa kusafirisha malighafi nje ya nchi, tunataka mwelekeo wetu uwe kwenye kuongeza thamani,” amesema.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa uliofanyika Mei 11 hadi 12, 2026 jijini Nairobi, Kenya.







Social Plugin