Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TADB YATOA GAWIO LA BILIONI 8.38 KWA SERIKALI


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa gawio la shilingi Bilioni 8.38 kwa serikali ikiwa ni ongezeko la Asilimia 50 kutoka shilingi Bilioni 5.58 ya mwaka 2024, katika Mkutano Mkuu wa wanahisa kwa mwaka ulioishia 31 Desemba 2025.

Akizungumza katika mkutano huo Msajili wa Hazina Bw. Nehemia Mchechu, ameipongeza TADB kwa kazi nzuri wanayofanya ya kutoa mikopo kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, na kusema kuwa ni Benki ya kimkakati hivyo serikali itaendelea kuiongezea mtaji.

“Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa serikali ni Benki ya kimkakati kwani kilimo kimeajiri watu wengi sana na ni sehemu kubwa ya uchumi, hivyo katika kuonesha dhana na umakini wa serikali kusimamia na kuinua kilimo, serikali itaendelea kuongeza mtaji ambapo mpaka sasa imekwisha wekeza jumla ya shilingi Bilioni 452.37 kama mtaji na tunategemea kuendelea kufanya uwekezaji uliomkubwa” amesema Nehemia Mchechu, Msajili wa Hazina.

Ameongeza kuwa, “Benki imeendelea kufanya vizuri kwani mwaka 2025 imezalisha faida kabla ya kodi ya shilingi Bilioni 35.45 ambayo ni kubwa kulinganisha na Bilioni 24.68 ya mwaka ulioishia Desemba 2024, Pamoja na faida waliozalisha wameleta serikalini gawio la shilingi Bilioni 8.38”.

Bw. Nehemia Mchechu ameishukuru bodi ya wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa TADB kwa kuendelea kuhakikisha uwekezaji wa serikali unaendelea kuimarika, hauyumbi, na Benki inazidi kukua na kuwafikia watu wengi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TADB, Bw. Ishmael Kasekwa amesema, Bodi ya Wakurugenzi inaihakikishia serikali (mwanahisa) kuwa itaendelea kuisimamia Benki kwa weledi ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

“Kwaniaba ya bodi ya wakurugenzi tunapenda kumhakikishia mwanahisa kuwa tutaendelea kuisimamia Benki ili iendelee kufanya vizuri katika utendaji wake na kutimiza malengo ambayo serikali ya Tanzania ilikusudia ilipoianzisha” amesema, Kasekwa.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege pamoja na kueleza mafanikio ya Benki kwa mwaka ulioishia Desemba 2025 pia ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuiunga mkono na kuhakikisha inatimiza malengo yaliyokusudiwa.

“Kutokana na ongezeko la utoaji mikopo kwa mwaka ulioishia Desemba 2025, faida baada ya kodi iliongezeka kutoka shilingi Bilioni 18.61 Desemba 2024 hadi kufika shilingi Bilioni 27.94 ikiwa ni ongezeko la asilimia 50” amesema Bw. Nyabundege.

Ameendelea Nyabundege “Katika mwaka ulioishia Desemba 2025, Kitabu cha Mikopo kimekua kutoka shilingi Bilioni 534.16 Desemba 2024 hadi kufikia shilingi Bilioni 806.75 Desemba 2025 sawa na ongezeko la Asilimia 51. Ongezeko hilo limechangiwa zaidi na upatikanaji warasilimali fedha, ongezeko la mtaji, mazingira wezeshi ya utendaji wa TADB na uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”.

TADB Kama Benki ya kisera tumekuwa tukiakisi kile kiongozi wa nchi na serikali imekuwa ikifanya, kama mlivyoshuhudia bajeti na uwekezaji kwenye kilimo umeongezeka hivyo na sisi tunajitahidi kuendana na kasi hiyo.

Sambamba na ongezeko la faida na utoaji mikopo thamani ya mali za Benki imekuwa kwa Asilimia 41 ukilinganishwa na mwaka ulioishia Desemba 2024.

“Katika mwaka ulioishia Desemba 2025, thamani ya mali za Benki ziliongezeka kutoka shilingi Bilioni 917.41 Desemba 2024 hadi shilingi Trilioni 1.3 sawa na ongezeko la asilimia 41”.

Aidha katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma zetu, kwa mwaka 2025 TADB iliongeza Ofisi 3 za Mikoa; Kigoma, Kagera na Ruvuma.

Nyabundege ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa jitihada mbalimbali inazozifanya Ili kuongeza ufanisi wa Benki, ikiwemo ongezeko la mtaji na mazingira wezeshi.

“Kwa niaba ya TADB napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiongezea Benki mtaji ambao umechangia moja kwa moja juhudi za Benki za kuleta mabadiliko na mapinduzi katika kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara”. Amesisitiza , Nyabundege.

“Napenda kuwakumbusha, TADB malengo yetu haswa ni kuhakikisha, tunachangia utoshelevu na usalama wa chakula nchini; pamoja na kuchagiza mapinduzi ya kilimo toka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara”.

“Ili kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja, kuongeza ajira na kupunguza umasikini, kuchukua hatua za kuhakikisha viatilifu na pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu, pamoja na kubainisha fursa za masoko ya mazao zilizoko ndani na nje ya nchi” amemalizia Bw. Nyabundege Mkurugenzi wa TADB.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com