SERIKALI imewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu na badala yake kuwapeleka kupata matibabu, elimu na huduma nyingine za msingi ili waweze kutimiza ndoto zao kama watoto wengine katika jamii.Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, Mei 30, 2026 alipotembelea Kituo cha Makazi ya Watoto Wenye Ulemavu cha Mlali kilichopo Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.
Akizungumza na wananchi, wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu, Mhe.Nderiananga amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma, hususan watu wenye ulemavu.
Amesema kundi hilo lina haki sawa na makundi mengine katika kupata elimu, matibabu, ulinzi na fursa mbalimbali za maendeleo.
Pia, amewataka wazazi kuacha kuona aibu au kuficha watoto wenye ulemavu, akisisitiza kuwa watoto hao wana vipaji, uwezo na mchango mkubwa kwa jamii endapo watapatiwa mazingira sahihi ya kukua na kuendelezwa.
“Msijifiche wala kuwafungia ndani watoto hawa. Watoeni wapate haki zao za msingi kama watoto wengine. Wana vipaji vikubwa na hakuna anayejua kesho yao. Inawezekana wakawa msaada mkubwa kwa familia na taifa hapo baadaye,” alisema.
Aidha, Mhe.Nderiananga amekemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wenye ulemavu na kueleza kuwa baadhi ya matukio hayo yamekuwa yakifichwa na familia badala ya kuripotiwa kwa Mamlaka husika.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Sozi Ngate, amesema Serikali imeendelea kushirikiana kwa karibu na kituo hicho kutokana na mchango wake mkubwa katika kuwahudumia watoto wenye ulemavu pamoja na kusaidia jamii inayokizunguka kupitia huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Makazi ya Watoto Wenye Ulemavu cha Mlali, Fr. Gaudence Aikaruwa, amesema kituo hicho kinatoa huduma za matibabu, upasuaji na elimu kwa watoto wenye ulemavu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Amsema kituo hicho kina uwezo wa kuhudumia watoto 75 kwa wakati mmoja wa jinsia zote, wenye umri wa kuanzia miaka mitatu hadi 12, bila kujali dini, kabila au mahali wanapotoka.
Katika kuonesha mshikamano na kuthamini huduma zinazotolewa katika kituo hicho,Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Kizito Wambura amesema, Serikali imekabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo mchele, sukari, maharage, mafuta ya kupikia, sabuni, nepi za watoto, viazi mviringo pamoja na vifaa vya michezo kwa ajili ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho.








Social Plugin