
Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa mgodi wa Barrick North Mara Francis Uhadi akizungumza
-Mabwawa yake ya takasumu yana viwango vya usalama vya kimataifa
Mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara unaendelea na kliniki ya siku saba ya kusikiliza malalamiko,kero na migogoro ya wananchi ili kupata utatauzi wa kudumu kwenye vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo ambapo pia kuwaelimisha shughuli mbalimbali za mgodi vilevile kutoa ufafanuzi wa maswali yanayoulizwa na wananchi yakiwemo yanayohusiana na usalama wa maji katika maeneo yao.
Kliniki hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele wiki iliyopita, inajumuisha wajumbe kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mgodi wa Barrick North Mara, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, asasi kiraia na wadau wengine, imelenga kuimarisha uhusiano kati ya mgodi na wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo hilo ili kuwezesha uwekezaji endelevu wenye manufaa kwa pande zote.
Akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa Kijiji cha Matongo ambao baadhi yao walikuwa na hofu ya maji ya chemichemi wanayoyaona katika maeneo yao kipindi hiki cha mvua na kuhofia kuwa yanatiririka kutoka mgodini, Meneja Msaidizi wa Idara ya Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara Nasieku Kisambu, alisema hakuna maji yoyote yanayotiririka kutoka mgodini kwenda kwa wananchi kutokana na mgodi kuwekeza kujenga bwawa la kuhifadhi mabaki ya taka zinazotokana na mchakato wa uzalishaji dhahabu (Tailings Storage Facility) kwa viwango vya kimataifa kuzingatia Afya na Usalama na kuendana na sheria za nchini.
“Bwawa la kuhifadhi taka sumu la mgodi wa Barrick Mara lina viwango vya kimataifa vya Afya na usalama ili kuzuia kemikali na tope sumu kutiririsha maji na kuingia katika mazingira ya jamii inayoizunguka Mgodi na linaendeshwa kwa usimamizi wa karibu na Mgodi na Mamlaka za Serikali ikiwemo Baraza la Taifa la Kuhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuhakikisha halileti madhara yoyote kwenye jamii”, alifafanua.
Vilevile alifafanua kwamba kampuni pia imewekeza katika ujenzi wa mitambo ya kisasa inayotibu maji machafu kutoa kwenye shughuli za uzalishaji ili yafae kutumika tena ndani ya mgodi na kurudishwa kwenye matumizi ya kawaida.
Naye Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhandi aliwaeleza wanakijiji cha Matongo jitihada mbalimbali zinazofanywa na mgodi kudhibiti changamoto ya vumbi katika maeneo hayo ikiwemo kumwaga maji kwenye maeneo yanayotoa vumbi kwenye maeneo yao ili kulinda Mazingira na Afya kwa wananchi.
Uhadi amesema kwamba kuna wataalamu ndani ya mgodi huo ambao hupita mara kwa mara kwa ajili ya ukaguzi pamoja na uchambuzi wa visima vya maji ya kunywa na vyanzo vya maji ya juu ya ardhi vinavyozunguka maeneo ya mgodi huo.
Barrick yenye ubia na Serikali nchini kupitia kampuni ya Twiga ilitumia zaidi ya dola za kimarekani milioni 65 katika mradi wa kujenga bwawa hilo la kuhifadhi taka sumu na kuongeza uwezo wa mtambo wa kusafisha maji mara 16 kutoka lita milioni 2.5 kwa siku hadi lita milioni 40 kwa siku hatua ambayo imepunguza kiasi cha chumvi katika maji machafu na kuwezesha kuhifadhiwa kwa usalama.
Urekebishaji TSF North Mara ulikamilika mwishoni mwa mwaka 2021.
Mradi wa maji safi ya kunywa vijiji vinavyozunguka mgodi
Katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata maji safi na salama , Mgodi wa Barrick North Mara kupitia fedha za CSR umefanikisha kutekelezwa kwa mradi wa maji chini ya usimamizi Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wenye thamani shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya upanuzi wa chanzo cha maji cha Nyamongo kilichopo ndani ya eneo la mgodi ambacho kilisanifiwa kuhudumia wananchi 27, 742 wa vijiji vya Nyangoto , Matongo , Mjini kati na Nyabichune.
Lakini kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji katika vijiji vingine saba vinavyozunguka mgodi. Chanzo hicho kilisanifiwa upya kwa lengo la kuhudumia wananchi 125,566 katika vijiji vingine sita vya Genkuru, Nyamwaga, Nyakunguru, Kerende, Msege na Komarera.
Mradi huo unaendelea kujengwa ambapo ukikamilika utamaliza tatizo la kupata maji salama katika vijiji hivyo.



Social Plugin