
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewahimiza Watanzania kulinda na kutunza amani kwa wivu mkubwa ili kuwezesha nchi kufikia malengo yake ya kimaendeleo.
Akizungumza na waandishi pamoja na maofisa habari mkoani Njombe, Msigwa alisisitiza kuwa hakuna nchi duniani iliyowahi kupata maendeleo ya kweli ikiwa wananchi wake wanavurugana na kugombana kila kukicha.
Alieleza kuwa ni jukumu la kila mwananchi kukataa hamasa zozote zinazoashiria fujo na vurugu, akionya kuwa mabeberu bado hawajalala na mara nyingi hutumia baadhi ya Watanzania miongoni mwetu kufanikisha ajenda zao za kuvuruga nchi.
Msigwa alifafanua kuwa ni vigumu kupiga hatua za kiuchumi ikiwa jamii itajikita kwenye maandamano ya kila siku na uharibifu wa miundombinu ambayo ndiyo uti wa mgongo wa biashara na usafirishaji.
Alitolea mfano wa wakulima wa maparachichi mkoani Njombe ambao wanategemea utulivu ili kuzalisha, akibainisha kuwa vitendo vya kuchoma bandari au viwanja vya ndege vinavyohamasishwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii vitaathiri uwezo wa kusafirisha bidhaa hizo kwenda nje ya nchi.
Aliongeza kuwa uharibifu wa mali za umma, kama mabasi ya mwendokasi, unamuumiza mwananchi wa kawaida ambaye kesho yake atakosa usafiri wa kumuwezesha kufanya kazi zake za kila siku.
Katika kulinganisha na hali ya kimataifa, Msemaji huyo wa Serikali alikumbusha madhara makubwa ya vita yanayoendelea katika nchi za Israel na Iran, akieleza namna mataifa hayo yanavyorudi nyuma kimaendeleo kutokana na ukosefu wa utulivu.
Aliwataka maofisa habari nchini kote kuendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kudumisha mshikamano. Alisisitiza kuwa utulivu wa nchi ndio msingi pekee utakaowezesha utekelezaji wa ndoto kubwa za Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Social Plugin