Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PUUZENI UONGO WA MITANDAONI KUHUSU BUNGE LA ULAYA NA RAIS SAMIA



Serikali kupitia Idara ya Habari - MAELEZO imetoa kanusho dhidi ya taarifa inayosambazwa mitandaoni ikidai kuwa Bunge la Ulaya limetoa maazimio ya kuondolewa kwa nguvu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Idara hiyo imebainisha wazi kuwa taarifa hizo ni uongo na upotoshaji unaopikwa na baadhi ya wanaharakati wa mitandaoni kwa lengo la kuzua taharuki isiyo na msingi miongoni mwa jamii.

Taarifa hiyo ilisema kwamba Video inayotumika kusambaza uongo huo ni ya tarehe 26 Novemba, 2025, na haihusiani kabisa na madai yanayotolewa, kwani Bunge la Ulaya haliendeshi mjadala wowote wa aina hiyo wala hakuna maazimio kama hayo yaliyofikiwa dhidi ya Tanzania.

Aidha taarifa hiyo imewataka wananchi kupuuza uongo huo wa mitandaoni ambao una dhima ya wazi ya kukwamisha juhudi kubwa zinazofanywa na Watanzania katika kuleta mshikamano, maridhiano, na kuondoa chuki miongoni mwetu.

"Serikali inaendelea kuwasihi Watanzania wote kuepukana na usambazaji wa taarifa hizi za upotoshaji ambazo zinachochea mifarakano na kudhoofisha umoja wa kitaifa. Ni muhimu kwa kila mwananchi kuwa mzalendo na kulinda amani iliyopo kwa kutozingatia uvumi unaolenga kurudisha nyuma hatua za maridhiano zilizofikiwa kwa maslahi ya taifa zima." ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com