
Na OWM - TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewasisitiza washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Afua ya Uthibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Miji, kuhakikisha suala usafi wa mazingira linakuwa ajenda ya kudumu katika vikao vyote vitakavyofanyika katika ngazi zote za Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwezesha miji na majiji nchini kuwa masafi.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Mei 12, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Mwaka wa Tathmini ya Afua ya Uthibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Miji, unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Jiji- Mtumba, unaohudhuriwa na Maafisa Afya wa Mikoa, Maafisa Afya wa Halmashauri na Maafisa Mazingira wa Halmashauri.
“Nasisitiza suala la usafi wa mazingira liwe ajenda ya vikao vyenu. Vikao vya Kamati za Ushauri za Mikoa, Kamati za Ushauri za Wilaya, Kamati za Maendeleo za Kata, Mabaraza ya Madiwani, Kamati za Kudumu za Halmashauri pamoja na vya ALAT ngazi ya mkoa na taifa,” amesema Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe ameainisha kuwa, usafi wa mazingira ukizingatiwa katika ngazi zote za Mamlaka ya Serikali za Mitaa utapunguza milipuko ya magonjwa na matumizi ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawa, na fedha zitakazookolewa zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo amewataka maafisa hao kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kupunguza milipuko ya magonjwa na matumizi ya ununuzi wa dawa.
“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuanzisha vitengo vya udhibiti wa taka ngumu ambavyo vinasaidia kuboresha zoezi la usafi wa mazingira nchini,” Prof. Shemdoe ameeleza.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Prof. Tumaini Nagu amesema uthibiti wa taka kwenye halmashauri ni jambo muhimu katika kuhakikisha kunakuwa na usafi wa mazingira na udhibiti wa magonjwa ya milipuko na kuongeza kuwa, takwimu za kisayansi zinaeleza kwamba uthibiti madhubuti wa taka ngumu unapelekea kupungua kwa asilimia 30 hadi 40 za magonjwa kama Malaria na mengineyo ambayo yanadhibitiwa kwa usafi wa mazingira.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti taka ngumu wa Halmashauri ya wilaya Bahi Bw. William Mpangala amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa inaendelea kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa afua za udhibiti wa taka ngumu kama za ukusanyaji na uchakataji wa taka ngumu, na kuongeza kuwa ushirikishwaji huo umeongeza ufanisi katika udhibiti wa taka kwenye halmashauri nchini.
Mkutano wa Mwaka huu una kaulimbiu isemayo “Taka ngumu ni Mali; tumia, rejeleza na Weka Miji katika hali ya usafi”.











Social Plugin