Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PPP YASAIDIA KUONGEZA UFANISI WA HUDUMA ZA HIJJA SAUDI ARABIA


Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) amesema mfumo wa ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP) umechangia kwa kiwango kikubwa kuongeza ufanisi wa huduma kwa mahujaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Abdulaziz (KAIA) uliopo Jeddah, Saudi Arabia, baada ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa Hajj Terminal.

Katika ujumbe wake aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X sambamba na salamu za Sikukuu ya Eid al-Adha, Mkurugenzi huyo alisema moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili mahujaji kwa miaka mingi ilikuwa muda mrefu wa kukamilisha taratibu za usafiri katika uwanja huo, ambapo baadhi yao walilazimika kutumia kati ya saa sita hadi kumi kabla ya kuendelea na safari za ibada ya Hijja.

Alieleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ya Saudi Arabia ilitekeleza mradi wa upanuzi wa Hajj Terminal kupitia mfumo wa PPP wenye thamani ya dola milioni 249, uliosainiwa mwishoni mwa mwaka 2006 na kukamilika mwaka 2011.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, mradi huo ulitekelezwa chini ya mkataba wa miaka 20 kati ya Mamlaka ya Anga ya Saudi Arabia (GACA) na kampuni binafsi ya Hajj and Umrah Terminals Development Company, muungano ulioongozwa na Saudi Binladin Group kwa kushirikiana na Aéroports de Paris Management, huku Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), mwanachama wa Benki ya Dunia, likiwa mshauri mwelekezi wa mradi huo.

Mkurugenzi huyo alisema kuanza kwa uendeshaji wa terminal hiyo kwa mfumo wa PPP kulileta maboresho makubwa ya kiutendaji, ambapo uwezo wa kuhudumia abiria kwa saa uliongezeka kutoka wastani wa abiria 1,000 hadi 1,500 kabla ya PPP na kufikia zaidi ya abiria 8,000 kwa saa baada ya maboresho hayo.

Aidha, alisema uwezo wa kuhudumia abiria kwa siku uliongezeka kutoka wastani wa abiria 25,000 hadi 30,000 kabla ya mfumo huo hadi zaidi ya abiria 91,000 wanaowasili na 84,000 wanaoondoka kwa siku katika kipindi cha msimu wa kilele wa Hijja.

Kwa upande wa uwezo wa mwaka, alieleza kuwa idadi ya mahujaji waliokuwa wakihudumiwa iliongezeka kutoka wastani wa milioni moja kwa mwaka hadi kati ya abiria milioni nane na tisa, huku terminal hiyo ikihudumia takribani mahujaji milioni 8.8 mwaka 2015.

Vilevile, alisema muda wa kukamilisha taratibu za usafiri uwanjani ulipungua kwa kiwango kikubwa kutoka saa sita hadi kumi kabla ya maboresho hadi kati ya dakika 45 na saa moja baada ya mfumo wa PPP kuanza kutumika.

“Mfumo wa PPP umeonyesha uwezo mkubwa wa kuongeza ufanisi kwa kupunguza muda wa huduma na kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria kwa kiwango kikubwa,” alinukuliwa akieleza katika ujumbe huo.

Akihitimisha ujumbe wake, Mkurugenzi huyo aliwatakia Waislamu heri ya Sikukuu ya Eid al-Adha huku akisisitiza kuwa uzoefu wa Saudi Arabia ni funzo muhimu kwa Tanzania kuhusu namna ubia kati ya sekta ya umma na binafsi unavyoweza kusaidia kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga na kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kiutendaji nchini.

Aliongeza kuwa tathmini ya sekta ya usafiri wa anga duniani ya mwaka 2023 ilionesha kuwa ingawa viwanja vya ndege vinavyoendeshwa kwa mfumo wa PPP ni takribani asilimia 14 pekee duniani, ndivyo vinavyohudumia karibu asilimia 40 ya abiria wote wa usafiri wa anga duniani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com