Mkurugenzi wa kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na binafsi (PPPC), David Kafuila amesema ubora wa rasilimali watu hususan afya na maarifa ndiyo “sarafu” ya dunia ya sasa, akieleza kuwa Tanzania haiwezi kufikia lengo la kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 bila kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya na wauguzi.
Kafulila amesema wauguzi ni nguzo muhimu ya rasilimali watu na mhimili mkubwa wa safari ya Tanzania kuelekea uchumi mkubwa, kwani afya bora ndiyo msingi wa uzalishaji, tija kazini na maendeleo ya taifa.
Amesema kazi ya uuguzi si ajira ya kawaida bali ni wito unaohitaji utu, subira na kujitoa kwa kiwango cha juu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi.
“Wauguzi ni daraja kati ya wagonjwa na kupona. Wapo mstari wa mbele kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora, jambo ambalo ni muhimu katika kujenga uchumi imara,” amesema Kafulila.
Amesema pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya afya, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba pamoja na kuongeza wataalamu wa afya, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya uwiano mdogo wa wauguzi kwa idadi ya watu.
Kafulila amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwepo kwa wauguzi 45 kwa kila watu 10,000, huku wastani wa Afrika ukiwa wauguzi 18 kwa watu 10,000, wakati baadhi ya nchi zilizoendelea zimefikia wauguzi 100 kwa watu 10,000.
Amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika kada ya uuguzi ili Tanzania iweze kufikia malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amesema Serikali pekee haiwezi kubeba mzigo wa maendeleo ya sekta ya afya, hivyo mchango wa sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Kafulila, takwimu zinaonesha kuwa sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya gharama za Mpango wa Taifa wa Maendeleo katika kipindi cha mwaka 2026/27 hadi 2030/31, huku zaidi ya asilimia 50 ya matumizi ya afya nchini yakitokana na sekta hiyo.
Amesema takribani asilimia 40 ya vituo vya afya nchini vinamilikiwa au kuendeshwa na sekta binafsi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
Kafulila amesema pamoja na juhudi hizo, bado kuna changamoto ya ongezeko kubwa la watu ambalo linaathiri uwezo wa Serikali kutoa huduma bora za afya na elimu kwa wananchi wenye kipato cha chini.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia uzazi wa mpango sambamba na juhudi za Serikali za kufungua uchumi na kuvutia uwekezaji, ili rasilimali zilizopo ziweze kutumika kwa ufanisi katika kuboresha maisha ya Watanzania.
“Wauguzi ndio uhai wa sekta ya afya. Uwekezaji katika wauguzi ni uwekezaji katika uchumi wetu. Kadiri uchumi unavyokuwa mkubwa, ndivyo ubora wa maisha ya wauguzi na wananchi kwa ujumla unavyoweza kuimarika,” amesema.

Social Plugin