Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTWARA YAFUNGUA FURSA MPYA KATIKA SEKTA YA CHUMVIMTWARA YAFUNGUA FURSA MPYA KATIKA SEKTA YA CHUMVI

- Serikali yapunguza gharama za leseni ya Madini Chumvi, wachimbaji wanufaika

📍Mtwara

Mkoa wa Mtwara umeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji katika sekta ya chumvi kutokana na uwepo wa fukwe zinazofaa kwa uzalishaji, maboresho ya mazingira ya biashara na ongezeko la uzalishaji linalofikia takribani tani 90 kwa majaruba manne katika baadhi ya maeneo ya uzalishaji.

Kutokana na hatua hiyo, wachimbaji na wazalishaji wa chumvi wameanza kunufaika na fursa mpya za kiuchumi kupitia kuongezeka kwa uzalishaji, ajira na upanuzi wa maeneo ya uzalishaji.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Winnifrida Mrema, amesema sekta ya chumvi mkoani humo inaendelea kukua kwa kasi kutokana na kuimarika kwa shughuli za uzalishaji pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchakataji wa chumvi.

Amesema maboresho hayo yanalenga kuongeza ubora wa chumvi kwa matumizi ya majumbani, viwandani na mifugo, huku yakichochea ajira kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka mashamba ya chumvi.

“Mtwara ina mazingira rafiki kwa uzalishaji wa chumvi na Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta hii ili kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Mrema.

Katika Kijiji cha Mnete, Kata ya Nalingu Halmashauri ya Mtwara Vijijini, msimamizi wa mashamba ya chumvi, Salum Amani, amesema mashamba hayo yanamilikiwa na Zamda Khatibu na yana leseni mbili za uvunaji chumvi pamoja na majaruba 24 yanayotumika kwa uzalishaji.

Amesema kwa sasa wanaendelea na shughuli za usafishaji wa majaruba baada ya msimu wa mvua ili kuruhusu maji ya chumvi kuingia tayari kwa uzalishaji mpya.

Kwa mujibu wa Salum, uzalishaji wa chumvi hutegemea hali ya hewa, ambapo jua kali huwezesha chumvi kukauka ndani ya siku 30, huku hali ya baridi ikifanya mchakato huo kuchukua hadi siku 40.

“Kwa kawaida majaruba manne huzalisha takribani tani 90 za chumvi kwa msimu mmoja, huku shughuli hizi zikitoa ajira kwa wafanyakazi tisa katika eneo hili,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Mkoa wa Mtwara na  Mwenyekiti wa Kamati ya Chumvi kupitia  FEMATA, Khalfan Nassoro, amesema kupunguzwa kwa gharama ya ada ya pango ya leseni za chumvi  kutoka Shilingi 45,000 hadi Shilingi 20,000 kumeongeza uwezo wa wazalishaji kupanua maeneo ya uzalishaji.

Amesema hatua hiyo imeongeza matumaini kwa wawekezaji na wachimbaji wadogo, huku akisisitiza kuwa mazingira bora ya uwekezaji yataifanya Mtwara kuwa kitovu kikuu cha uzalishaji wa chumvi nchini.

Nassoro amesema pia ukuaji wa sekta hiyo unaweza kuchochea ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya chumvi na hivyo kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com