Imebainika kuwa uwepo wa michakato miwili inayoweza kuendeshwa kwa wakati mmoja, yaani Tume ya Uchunguzi wa Kijinai na mchakato wa Maridhiano ya Kitaifa, hauwezi kusababisha mwingiliano au mgongano wa kiutendaji ndani ya serikali.


Wataalamu wa sheria na masuala ya kikatiba wanafafanua kuwa kila mchakato unaendeshwa kwa uhuru wake na hakuna unaoweza kuathiri hatua za mwingine.

Ingawa inawezekana kisheria michakato hii kwenda sambamba au mmoja kutangulia, wataalamu wanashauri kuwa ni vyema Tume ya Uchunguzi wa Kijinai ikaanza mapema ili kuweka msingi wa ukweli wa kisheria kabla ya kuelekea kwenye hatua za maridhiano.

Baada ya Tume ya Kijaji kukamilisha kazi yake chini ya kifungu cha 21 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, inawasilisha taarifa hiyo kwa Rais ambaye anayo mamlaka makubwa ya kisheria kuamua kuweka wazi taarifa hiyo au kuishikilia kwa siri.

Rais anaweza kuelekeza kuchukuliwa hatua za kijinai kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na Jeshi la Polisi, au hatua za kiutawala na kinidhamu, pamoja na kuamuru ulipaji wa fidia kwa waathirika.

Kupitia ripoti hiyo, Rais pia anayo Mamlaka ya Kipekee ya Kikatiba, ikiwemo mamlaka ya kutoa msamaha, ili kuangalia uwiano wa makosa dhidi ya ubinadamu na maslahi mapana ya nchi katika mabaraza ya kimataifa, hivyo kufanya mchakato wa maridhiano kuwa na tija bila kuathiri utekelezaji wa sheria.