
Mwanaume mmoja aitwaye Kasese Gerevas Bilalo (47), ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Habari Njema na Mkazi wa Kijiji cha Nyarututu, Kata ya Bwanga, Wilaya ya Chato mkoani Geita, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe, Martha Faustine (45), Mkazi wa Wilaya ya Chato Mkoani humo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la mauaji ambapo amesema chanzo kinadaiwa kuwa ni migogoro ya kifamilia iliyotokana na marehemu kumtuhumu mumewe kuwa na mahusiano ya nje ya ndoa, hali iliyosababisha migogoro ya mara kwa mara katika familia hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda SACP Jongo, tukio hilo limetokea Mei 12, 2026, majira ya saa sita mchana katika Kijiji cha Nyarututu, Kata ya Bwanga, Wilaya ya Chato, ambapo marehemu alikutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yao katika mazingira ambayo Jeshi la Polisi limeeleza kuwa yalitengenezwa ili kuonekana tofauti na uhalisia.
Aidha, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alimvizia mkewe akiwa amelala, kisha akamkaba shingoni kwa kutumia kamba ya katani kabla ya kumning’iniza juu ya kenchi ili tukio hilo lionekane kama la kujinyonga.
Kamanda SACP Jongo amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kukamilishwa ili mtuhumiwa afikishwe kwenye mamlaka husika za kisheria.
Social Plugin