
Serikali imetangaza hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi nchini, ambapo upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa urefu wa kilomita 1,000 umekamilika, ukiunganisha maeneo ya kimkakati yakiwemo matawi ya kuelekea miradi ya Liganga na Mchuchuma.
Hatua hii inakwenda sambamba na maandalizi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Njombe, ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho za kuwalipa fidia wananchi watakaopisha mradi huo ili kuruhusu ujenzi kuanza mara moja.
Taarifa ya maendeleo hayo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe.
Akizungumza kutoka katika mashamba ya Njombe alisema maendeleo hayo ya miundombinu yanahusisha pia maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Songea ambao tayari umewekwa mifumo ya taa, hali inayowezesha ndege kutua na kuruka wakati wowote, mchana na usiku, na hivyo kuchochea shughuli za usafiri na biashara katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Katika kuimarisha usafirishaji wa mizigo mizito, ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara unaendelea kwa kasi kwa lengo la kuhudumia shehena mchanganyiko (dry bulk cargo) kama vile makaa ya mawe na saruji, jambo litakalopunguza gharama za usafirishaji kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
Aidha, ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay unaendelea vyema huku reli ya TAZARA ikitarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa ambapo tayari Mkandarasi kutoka kampuni ya CCECC ya nchini China yupo kazini.
Mageuzi haya ya miundombinu yanatajwa kuwa mhimili mkuu wa mafanikio ya miradi ya kitaifa ya kielelezo kama Liganga na Mchuchuma, kwani yatasaidia kusafirisha tani milioni 1.1 za bidhaa za chuma na tani milioni 3 za makaa ya mawe zitakazozalishwa kwa mwaka kuelekea kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi. 






Social Plugin