Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KILA AWAMU YA UTAWALA INA MCHANGO WAKE KATIKA UJENZI WA TAIFA

Tanzania tangu ilipopata uhuru mwaka 1961 imepitia hatua mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Mabadiliko hayo yamechangiwa na mifumo tofauti ya kiuchumi, kisiasa pamoja na mabadiliko ya dunia kwa ujumla.

 Katika kipindi hicho, taifa limejenga msingi wa umoja, amani, elimu, miundombinu na uchumi, huku kila awamu ya uongozi ikiwa na mchango wake katika maendeleo ya nchi.

Mfumo wa Uchumi Tanzania Baada ya Uhuru

Kuanzia mwaka 1967 hadi 1985, Tanzania ilifuata mfumo wa uchumi dola (Centralized Economy) chini ya sera ya Ujamaa na Kujitegemea iliyotangazwa kupitia Azimio la Arusha. Mfumo huo uliweka umiliki mkubwa wa serikali katika viwanda na nyenzo za uzalishaji.

Katika kipindi hicho, serikali ilisimamia viwanda mbalimbali ikiwemo Urafiki Textile (Dar es Salaam), MWATEX (Mwanza), MUTEX (Musoma) na Mtibwa Sugar (Morogoro). Lengo kuu lilikuwa kujenga taifa linalojitegemea kiuchumi na kupunguza utegemezi kutoka nje.

Hata hivyo, kutokana na changamoto za uchumi wa dunia pamoja na ushawishi wa taasisi za kifedha za kimataifa kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF), Tanzania ilianza kufanya mageuzi ya kiuchumi.

Kuanzia mwaka 1986, taifa lilianza mfumo wa uchumi wa kiliberali maarufu kama “Ruksa”, ambapo wananchi walipewa uhuru mkubwa zaidi wa kufanya biashara, kuanzisha viwanda, kampuni binafsi na taasisi mbalimbali za elimu na huduma.

AWAMU ZA UONGOZI NA MCHANGO WAKE KATIKA MAENDELEO YA TAIFA

Awamu ya Kwanza: Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1961–1985)

Hayati Mwalimu Julius Nyerere ndiye Baba wa Taifa na kiongozi aliyeweka msingi mkubwa wa taifa la Tanzania. Mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni mkubwa na wa kihistoria.

Mchango wake:

  1. Alipigania na kuiongoza Tanzania kupata uhuru mwaka 1961.

  2. Aliunganisha Watanzania kupitia matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya taifa.

  3. Aliasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

  4. Alianzisha sera ya Ujamaa na Kujitegemea kupitia Azimio la Arusha mwaka 1967.

  5. Alianzisha mfumo wa uchumi dola kwa lengo la kujenga taifa linalojitegemea.

  6. Aliimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuondoa mifumo ya kikabila.

  7. Aliongoza vita dhidi ya Idi Amin wa Uganda na kulinda mipaka ya Tanzania.

  8. Alitaifisha baadhi ya shule binafsi ili kutoa fursa sawa ya elimu kwa wananchi wote.

  9. Alianzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kuzalisha wataalamu wa taifa.

  10. Alihimiza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kwa mtazamo wa kidemokrasia.

  11. Aliondoa mfumo wa utawala wa machifu kwa lengo la kujenga taifa lenye usawa.

Mwalimu Nyerere alijenga msingi wa amani, umoja na utaifa ambao unaendelea kuonekana hadi leo.

Awamu ya Pili: Hayati Ali Hassan Mwinyi (1985–1995)

Hayati Ali Hassan Mwinyi aliongoza kipindi cha mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini. Serikali yake ilifungua milango ya uchumi wa soko huria.

Mchango wake:

  1. Alianzisha mfumo wa uchumi wa kiliberali maarufu kama “Ruksa”.

  2. Alihimiza sekta binafsi kushiriki katika uchumi.

  3. Aliruhusu kuanzishwa kwa taasisi binafsi za elimu ya juu na biashara.

  4. Aliasisi mfumo wa vyama vingi vya siasa baada ya mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali.

  5. Aliimarisha diplomasia ya kimataifa na ushirikiano wa Tanzania na mataifa mengine.

  6. Katika uongozi wake, Papa John Paul II alifanya ziara nchini Tanzania mwaka 1990.

Awamu hii ilifungua nafasi kwa wawekezaji binafsi na kuongeza ushindani katika uchumi.

Awamu ya Tatu: Hayati Benjamin William Mkapa (1995–2005)

Hayati Benjamin Mkapa aliendeleza mageuzi ya kiuchumi na kuimarisha misingi ya utawala bora.

Mchango wake:

  1. Aliendeleza sera ya ubinafsishaji.

  2. Aliimarisha sera za utandawazi na uwekezaji.

  3. Alijenga miundombinu ya barabara na madaraja, ikiwemo Daraja la Mkapa.

  4. Alipunguza deni la taifa na kuimarisha uchumi.

  5. Alishiriki kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki.

  6. Alijenga majengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

  7. Alianzisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

  8. Alianzisha Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

  9. Alianzisha programu mbalimbali za kupunguza umaskini kama MKUKUTA, MKURABITA na MKUZA.

  10. Alijenga jengo la Bunge Dodoma pamoja na Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Utawala wake uliweka msingi mzuri wa usimamizi wa uchumi na mapato ya taifa.

Awamu ya Nne: Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (2005–2015)

Dkt. Jakaya Kikwete aliendelea kuimarisha sekta za elimu, afya na miundombinu.

Mchango wake:

  1. Aliunganisha mikoa mingi kwa barabara za lami, hatua iliyochochea biashara na usafirishaji.

  2. Serikali yake iliimarisha taasisi za TANROADS na TARURA kwa usimamizi wa miundombinu.

  3. Alijenga shule za sekondari karibu kila kata nchini, jambo lililopanua fursa za elimu.

  4. Alijenga hospitali na taasisi za afya za kisasa ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

  5. Alianzisha na kuimarisha huduma za afya katika Hospitali ya Mloganzila na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

  6. Alihamasisha kampeni za afya kwa wananchi na kuimarisha huduma za matibabu.

  7. Aliimarisha diplomasia ya kimataifa na kuvutia wawekezaji nchini.

Awamu hii iliongeza huduma za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo mengi.

Hitimisho

Kwa ujumla, Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii tangu kupata uhuru mwaka 1961. Kila awamu ya uongozi imechangia kwa namna yake katika kujenga taifa lenye umoja, amani na maendeleo.

Licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii, bado Tanzania imeendelea kupiga hatua katika sekta za elimu, afya, miundombinu, uwekezaji na huduma za jamii.

Ni wajibu wa Watanzania kuendelea kushirikiana, kufanya kazi kwa bidii na kulinda amani ya nchi ili kuhakikisha maendeleo haya yanaendelea kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Makala hii imeandikwa na
John Francis Haule
Mkuu wa Soko la Samunge
Jijini Arusha
SM 0756 717987 au 0711993907



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com