Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Serikali ya Tanzania zimefikia makubaliano katika ngazi ya wataalamu kuhusu ukamilishaji wa tathmini za mwisho za mpango wa ufadhili wa Dola za Marekani milioni 375.5 ambazo ni sawa na takriban Shilingi bilioni 974. Fedha hizi zitaingizwa nchini baada ya kuidhinishwa rasmi na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa programu za mikopo nafuu ambazo zimeisaidia nchi kupata zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja kwa ajili ya miradi ya kiuchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi tangu programu hizo zilipoanza.
Kiongozi wa timu ya wataalamu ya IMF, Nicolas Blancher, ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam kufuatia ziara ya tathmini ambapo amebainisha kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara huku mfumuko wa bei ukibaki ndani ya malengo yaliyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). IMF imeridhishwa na hatua za serikali katika kuimarisha ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na uwezo wa kukabili misukosuko ya kiuchumi duniani ikiwemo athari za vita vya Mashariki ya Kati kupitia usimamizi madhubuti wa sera za fedha.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameeleza kuwa serikali imefanikiwa kufikia malengo makuu ya kiuchumi yaliyowekwa kwenye programu hizo na itaendelea kusimamia matumizi ya fedha hizo kwa umakini mkubwa. Alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi na unaleta tija ya moja kwa moja katika sekta za uzalishaji na kutoa huduma bora za kijamii kwa wananchi wa Tanzania.
Ripoti ya wataalamu hao pia imeonesha kuwa serikali imeongeza matumizi katika sekta muhimu za elimu na afya huku kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kikibaki katika hali ya kuridhisha. Hatua hizi zimesaidia kujenga msingi imara wa uchumi ambao unatarajiwa kuendelea kukua kwa kasi ya asilimia 5.9 ifikapo mwaka 2026, jambo ambalo linaashiria utulivu na mwelekeo chanya wa maendeleo ya Taifa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Blancher alipongeza jitihada za Tanzania katika kuimarisha utulivu wa uchumi jumla na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji licha ya changamoto za kimataifa. Ushirikiano huu kati ya Tanzania na IMF unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha nchi inapata mitaji nafuu ya kusaidia ukuaji wa sekta mbalimbali na kujiandaa vyema dhidi ya hatari za kiuchumi na kimazingira zinazoweza kujitokeza siku za usoni.
Social Plugin