Afisa Uhamiaji Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Robert Mahenge akitoa elimu ya Uhamiaji, Uraia, Pasipoti na Hati za Safari kwa waumini wa kanisa la Romani catholic parokia ya yohana maria vianey Mhunze Wilayani humo Aprili, 12, 2026 kwenye ibada ya Misa Takatifu
Na Sumai Salum- Kishapu
Afisa Uhamiaji Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Robert Mahenge, ametoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya Uhamiaji, Uraia, Pasipoti na Hati za Safari, tukio lililofanyika Jumapili, Aprili 12, 2026, katika Kanisa la Roman Catholic Parokia ya Yohane Maria Vianney Mhunze.
Akizungumza na waumini mara baada ya Ibada ya Misa hiyo Takatifu, Mahenge amewahimiza wananchi kufuata sheria za nchi na kushirikiana na mamlaka za uhamiaji ili kulinda usalama na maslahi ya taifa.
Amesema kuwa wananchi, hususan walowezi, wanapaswa kufika katika Ofisi za Uhamiaji kuhakiki na kuhuisha taarifa zao mapema, hasa baada ya huduma hizo kusogezwa karibu katika Wilaya ya Kishapu, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma na ufuatiliaji wa taarifa sahihi.
Mahenge amesisitiza kuwa uzalendo wa kweli unaanzia kwa mwananchi mmoja mmoja, kwa kuwabaini na kutoa taarifa za wageni wanaoishi katika maeneo yao bila kufuata taratibu za kisheria.
Ameeleza kuwa bado kuna baadhi ya wananchi wanaowaingiza raia wa kigeni kwa kuoana, ajira au shughuli za kiuchumi kama kilimo na ufugaji bila kufuata sheria, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa jamii na nchi kwa ujumla.
“Ni muhimu kwa kila anayehusika na mahusiano, ajira au shughuli zozote zinazowahusisha raia wa kigeni kuhakikisha wanazingatia sheria na kupata vibali stahiki kutoka Idara ya Uhamiaji,” amesisitiza Mahenge.
Kwa upande wake, Padre Deusdedit Nkandi aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu, amewataka waumini kuwa mfano wa kuigwa kwa kuheshimu na kutii sheria za nchi.
Padre Nkandi amesisitiza kuwa kanisa lina wajibu wa kuwa kielelezo cha maadili mema, huku akiwahimiza walowezi na wananchi kwa ujumla kwenda kuhakiki taarifa zao mapema ili kuepuka matatizo ya kisheria.
Ameongeza kuwa kanisa linaunga mkono juhudi za serikali katika kuelimisha jamii kuhusu uzingatiaji wa sheria na kuimarisha uzalendo miongoni mwa wananchi.
Social Plugin