Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VYAMA 12 VYA SIASA VYAUNGA MKONO RIPOTI YA JAJI CHANDE, WAHIMIZA MARIDHIANO YA KITAIFA



Vyama 12 vya siasa nchini Tanzania vimejitokeza kwa pamoja na kupongeza ripoti ya Tume huru ya kuchunguza matukio ya Uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kutaka kuharakishwa kwa mchakato wa maridhiano na kupatikana kwa Katiba mpya kama ilivyopendekezwa na tume hiyo.

Leo Jumapili Aprili 26, 2026 Jijini Dar Es Salaam, mbele ya waandishi wa habari, vyama hivyo katika tamko lao la pamoja wamesema kitendo cha Tume hiyo kupendekeza mchakato wa Katiba kuanza kabla ya mwaka 2028 kunapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa kwani ndio suluhu ya changamoto za kisiasa na kijamii na Katiba mpya itaweka mustakabali mwema wa Tanzania.

Vyama hivyo vilivyoungana na kutoa tamko hilo ni DP, NRA, NLD, AAFP, Ada Tadea, Demokrasia Makini, UPDP, UDP, Sau, UMD, TLP na CCK ,wakisisitiza utayari wao katika kushirikiana na serikali kwenye utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyoainishwa na tume hiyo, kama sehemu ya kudumisha amani na utulivu na kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo nchini.

"Kupatikana kwa Katiba mpya hakutaondoa tu changamoto za kisiasa bali pia kutaliponya Taifa kwa changamoto mbalimbali inazozipitia. Tunawaambia watanzania kuwa tunaenda kuliponya Taifa kwa upatikanaji wa Katiba mpya na kuanza kwa mchakato wa maridhiano. Nchi itaendelea pia kuwa ya amani na yenye utulivu kupitia mambo haya." Amesema Hassan Doyo, Mgombea urais wa NLD 2025.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa hilo na Mgombea Urais katika uchaguzi Mkuu wa 2025 Bw. Abdul Muya kando ya kuipongeza Tume ya Jaji Mohamed Othman Chande, akitoa wito wa kuitishwa kwa Baraza la vyama vya siasa ili kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu kutoka kwenye ripoti hiyo ya Jaji Chande, akisisitiza pia vyombo vya dola kuanza kuchukua hatua kwa vichocheo vilivyotajwa kama sababu ya ghasia za Oktoba 2025.

Wakati wa hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, pamoja na mambo mengine alisisitiza ahadi yake wakati wa uchaguzi Mkuu ya kupatikana kwa Katiba mpya katika kipindi chake hiki cha pili, akitangaza pia kuunda Tume ya maridhiano hivi karibuni itakayosimamia mchakato wa kupatikana kwa maridhiano.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com