Tanzania imewasilisha kwa uthabiti mafanikio yake katika kuboresha sekta ya afya kupitia mageuzi ya kimkakati, ubunifu wa kidijitali, na uwekezaji wa ndani unaolenga kuokoa maisha.
Akiwasilisha taarifa hiyo katika mkutano unaofanyika 13- 17 Aprili 2026 nchini hapa, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed O. Mchengerwa alieleza hatua zilizopigwa na nchi na kusisitiza dhamira ya kumaliza vifo vinavyoweza kuzuilika vya akina mama na watoto wachanga.
Akizungumza kwa niaba ya serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, Mchengerwa alibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Alisema mageuzi hayo yamejikita katika kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha utoaji wa huduma, na kukuza ubunifu unaoleta matokeo halisi kwa wananchi.
“Tanzania imejipanga kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza maisha wakati wa kujifungua kwa sababu ya kukosa huduma muhimu au dawa za kuokoa maisha,” alisisitiza Mchengerwa.
Ikiwa na takribani watu milioni 62, Tanzania inaendelea kuweka kipaumbele katika bima ya afya kwa wote, afya ya uzazi, mama na mtoto, kuimarisha huduma za afya ya msingi, kudhibiti magonjwa, na kukuza rasilimali watu katika sekta ya afya. Lengo kuu ni kupunguza vifo vya mama na mtoto huku ikipanua upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote.
Sehemu muhimu ya mafanikio haya ni matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika utoaji wa huduma za afya.
Vituo vyote 8,382 vya afya vya umma vinatumia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa vifaa tiba (eLMIS), unaorahisisha uagizaji na usambazaji wa dawa na vifaa muhimu.
Mfumo huu umeunganishwa na mifumo mingine kama EPICOR 10 na DHIS2, hatua inayoboresha upangaji na usimamizi wa rasilimali za afya.
Aidha, kuna juhudi za kuunganisha mifumo ya GoTHOMIS na Afya eHMS, pamoja na kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa utoaji na usimamizi wa dawa.
Maboresho haya yanatarajiwa kuongeza usalama wa mgonjwa, kupunguza upotevu wa dawa, na kuimarisha uwajibikaji katika mnyororo mzima wa ugavi wa afya.
Ubunifu wa teknolojia pia unasaidia kukabiliana na changamoto za huduma katika maeneo ya mwisho (last mile).
Amesema Mfano ni mfumo wa usafiri wa dharura wa M-Mama ambao umeboresha rufaa kwa wajawazito na watoto wachanga, pamoja na mikutano ya kidijitali ya uchambuzi wa vifo vya mama na mtoto ambayo inaharakisha hatua za kuboresha huduma.
Ameongeza kuwa kutokana na mafunzo ya janga la UVIKO-19, Tanzania inaendelea kuimarisha uwezo wa mifumo yake ya afya kukabiliana na majanga yajayo.
Nchi inahamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya ili kuboresha upatikanaji na kupunguza utegemezi wa nje.
Mradi mkubwa katika eneo hili ni uanzishaji wa Ukanda Maalum wa Viwanda vya Dawa wa Mloganzila, unaolenga kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira, na kuimarisha uzalishaji wa dawa ndani ya nchi.
Amesema ili kuharakisha juhudi hizi, serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa (PIAT).
"Tanzania pia inatambua umuhimu wa ushirikiano wa kikanda. Kupitia Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), nchi inaunga mkono ununuzi wa pamoja wa dawa na imepewa jukumu la kuwa mwenyeji wa huduma hizi, hatua inayoongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya katika ukanda huo." Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Upande wa fedha, serikali inaendelea kuboresha bima ya afya kwa wote na kupunguza gharama kwa wananchi. Huduma zinazotolewa zinajumuisha dawa muhimu kwa afya ya mama na mtoto kama oxytocin, misoprostol, na amoxicillin.
Kupitia mbinu bunifu za kifedha kama ufadhili linganishi, mikopo ya muda, na fedha chachu, Tanzania inaimarisha upatikanaji endelevu wa huduma. Mwaka 2025, serikali ilitoa dola milioni 5.7 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za uzazi wa mpango, ikionyesha dhamira ya dhati ya kisiasa na umiliki wa ndani.
Mchengerwa alisisitiza kuwa matumizi ya takwimu sahihi ni msingi wa mafanikio haya. Kuunganishwa kwa mifumo ya DHIS2 na eLMIS kunasaidia kufuatilia upatikanaji wa dawa kwa wakati halisi, kuzuia upungufu, na kuboresha maamuzi ya upangaji.
“Takwimu bora zinawezesha maamuzi bora, mifumo imara ya ugavi, na hatimaye kuokoa maisha zaidi,” alieleza.
Aidha, amefafanua kuwa Tanzania imesisitiza kuwa ubunifu, uhuru wa kitaifa katika uzalishaji, na mifumo imara ya kifedha ni muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wote, hasa walio maeneo ya mbali.
Kupitia juhudi hizi, Tanzania inaendelea kujijengea nafasi kama kinara katika kuimarisha usawa wa afya na kulinda maisha ya mama na mtoto.





Social Plugin