Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAMCU YAIMARISHA UCHUMI WA WAKULIMA TUNDURU KWA UNUNUZI WA MALORI MAPYA MATANO

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Denis Masanja (wa tatu kutoka kulia), akikata utepe kuashiria makabidhiano ya malori matano mapya ya Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) Limited.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru (TAMCU), Musa Manjaule (kushoto), na Meneja Masoko wa Benki ya CRDB Kanda ya Kusini, Emanuel Bigailo, wakisaini hati ya makabidhiano ya malori matano mapya yaliyonunuliwa na TAMCU kwa mkopo kutoka CRDB. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Deni Masanja, akishuhudia tukio hilo.

Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma

Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru (TAMCU) kimechukua hatua kubwa ya kuongeza ufanisi katika sekta ya kilimo kwa kununua malori matano mapya ya kubebea mazao, hatua inayolenga kurahisisha usafirishaji na kuongeza mapato ya chama pamoja na wanachama wake.

Uamuzi huo umepokelewa kwa furaha na wakulima wa wilaya hiyo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya ucheleweshaji wa mazao kufika sokoni kutokana na uhaba wa vyombo vya usafiri.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima, Rashid Chibwana amesema kuwa malori hayo yatasaidia kuwafikia wakulima mashambani na kusafirisha mazao yao kwa wakati hadi maghala na hatimaye kwenye minada.

Amebainisha kuwa hapo awali walitegemea chanzo kimoja cha mapato, lakini uwekezaji huo mpya utaongeza mapato ya chama huku ukipunguza gharama na usumbufu wa usafirishaji.

Mwenyekiti wa TAMCU, Mussa Manjaule, amesema ununuzi wa malori hayo umetokana na maombi ya wanachama waliotaka kuboreshwa kwa huduma za usafirishaji pamoja na kuongeza vyanzo vya mapato.

Ameeleza kuwa awali walikuwa wanapata changamoto hata katika kusafirisha pembejeo kama viuatilifu kutoka mikoa jirani, lakini sasa hali hiyo itaboreshwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Tunduru, Emanuel Mwasuka, amesema benki hiyo imechangia sehemu kubwa ya fedha zilizotumika kununua malori hayo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5.

Ameahidi kuendelea kushirikiana na vyama vya ushirika kwa kutoa mikopo, huku akisisitiza umuhimu wa kuyatunza malori hayo ili yadumu na kuleta tija inayokusudiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja, ameipongeza TAMCU kwa hatua hiyo akieleza kuwa ni mfano bora wa maendeleo katika sekta ya ushirika.

Amesema uwekezaji huo utachochea biashara ya mazao kama korosho, ufuta na mbaazi, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza kipato kwa wakulima, huku akitoa wito kwa wanachama kushirikiana na viongozi wao ili kufanikisha malengo ya chama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com