
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO, Kelvin Kanje amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Wadau wa Habari ili kuendelea kuboresha sekta hiyo na hatimaye ipate mafanikio zaidi ya yaliyopo sasa.
Ameyasema hayo leo Aprili 29, 2026 katika hoteli ya Mount Meru iliyopo jijini Arusha wakati akitoa salamu kwenye Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyoanza Aprili 28, 2026.
"Nawashukuru wadau wa habari walioshiriki katika maadhimisho haya, naamini tutaendelea kushirikiana zaidi ili sekta hii iwe na mafanikio zaidi", amesema Kanje.
Akizungumza kuhusu chimbuko la uhuru wa vyombo vya habari, Mwakilishi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Michel Toto amesema kuwa miaka 35 iliyopita, wadau wa habari kutoka kote Afrika walikutana kuandaa wito wa uhuru wa vyombo vya habari, uliojulikana kama “Azimio la Windhoek kuhusu Kukuza Vyombo Huru na Vyenye Wingi Barani Afrika lililolenga kufanya mtiririko huru wa taarifa kuwa manufaa ya umma.
"Tunapoadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ninatoa wito kwa kila mtu kuhuisha dhamira yake kwa haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza, kuwatetea wafanyakazi wa vyombo vya habari, na kuungana nasi kuhakikisha kwamba taarifa zinaendelea kuwa rasilimali ya umma". ameongeza Bw. Toto.
Akizungumza kuhusu mabadiliko ya sekta ya habari, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tech & Media Convergency (TMC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Asha Abinallah amesema kuwa uandishi wa habari unapitia mabadiliko makubwa yanayosukumwa na teknolojia mpya, mabadiliko ya imani ya umma, changamoto za usalama, akili unde (AI), utegemezi wa majukwaa ya kidijitali, taarifa potofu pamoja na mifumo dhaifu ya biashara ya habari.
"Mabadiliko hayo yanalifanya jukwaa hili kuwa siyo sherehe tu ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani bali ni jukwaa la kazi la mijadala, kutambua changamoto na kuchora dira ya mustakabali wa sekta ya habari", amesema Bi. Asha.
Maadhimisho hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa kesho Aprili 30, 2026, yanaongozwa na kaulimbiu inayoesema ‘Kujenga Mustakabali wa Amani, Kukuza Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa ajili ya Haki za Binadamu, Maendeleo na Usalama’.
Picha : MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI 'World Press Freedom Day 2026'
Social Plugin