
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Kagera, Ndugu Erick Peter Makundi, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka malimbikizo pamoja na usumbufu unaoweza kujitokeza baadaye.
Amesisitiza kuwa ulipaji wa kodi hiyo si hiari, bali ni wajibu wa kila mmiliki wa ardhi, na unachangia moja kwa moja katika kuboresha huduma za kijamii zinazotolewa na serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Aprili 29, 2026, Makundi alisema Mkoa wa Kagera umejipanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 4.1 za kodi ya pango la ardhi katika kipindi hiki cha ukusanyaji wa mapato.
Alieleza kuwa kufikiwa kwa lengo hilo kutasaidia kuongeza mapato ya serikali na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Makundi alibainisha kuwa serikali imeweka sheria madhubuti kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi, ikiwemo kufutiwa hati za umiliki wa ardhi au kuchukuliwa hatua za kisheria mahakamani.
Hivyo aliwasisitiza wananchi kutekeleza wajibu wao kwa hiari na kwa wakati ili kuepuka hatua hizo ambazo zinaweza kuathiri umiliki na matumizi ya ardhi zao.
Aidha, alifafanua kuwa wananchi wanaoshindwa kulipa kodi kwa wakati wanaweza kukumbana na changamoto mbalimbali, zikiwemo kushindwa kutumia hati zao za ardhi kupata mikopo au kuzitumia kama dhamana hadi watakapomaliza kulipa madeni yao.
Aliongeza kuwa ulipaji wa kodi kwa wakati ni sehemu ya uwajibikaji wa kila mwananchi katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kagera, akiwemo Ndg. Johnsen Mgisha mkazi wa Kata ya Kashai pamoja na Ndg. Audax Matias kutoka Kata ya Bakoba, wamesema wamepokea wito huo kwa mtazamo chanya na wako tayari kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati. Hata hivyo, wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kodi ya ardhi na kuboresha mifumo ya ulipaji ili iwe rahisi zaidi kwa wananchi wote.
Kwa ujumla, mpango wa Mkoa wa Kagera wa kukusanya shilingi bilioni 4.1 za kodi ya pango la ardhi unaonyesha dhamira ya serikali katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuongeza uwezo wa kugharamia huduma za maendeleo. Wananchi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha azma hiyo kwa kulipa kodi kwa wakati, kwa kuwa maendeleo ya taifa yanategemea mchango wa kila mmoja.






Social Plugin