Na mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumapili Aprili 26, 2026 katika kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanzania ametangaza msamaha kwa wafungwa 1,369 kati yao 436 wakiachiwa huru na wafungwa wengine 933 wakipunguziwa adhabu zao na kubaki gerezani ili kuendelea kutumikia sehemu ya vifungo vilivyosalia.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mhe. Paschal Katambi Patrobas imesema ni matarajio ya serikali kuwa wafungwa walioachiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena kwenye vifungo gerezani.
Kulingana na taarifa ya Wizara, wafungwa walionufaika na msamaha huo ni wale wanaotumikia kifungo cha mwaka mmoja na kuendelea, waliotumikia robo ya adhabu ya kifungo gerezani na wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu (sugu) ambao wapo katika hatua za mwisho na waliothibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa wilaya.
Msamaha huo pia umewahusu wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini na kuendelea, waliothibitishwa na jopo la waganga, wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wale wenye ulemavu wa mwili na akili kwa kuthibitishwa na jopo la Waganga na wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini (under Presidential pleasure) ambao wamekaa gerezani miaka kumi au zaidi.
Wengine ni wafungwa wa kunyongwa waliokaa gerezani miaka 15 na kuendelea, kuanzia tarehe ya kuanzia tarehe ya kuanza kifungo ambao taratibu za rufaa zimekamilika na mashauri yao kutolewa uamuzi/hukumu, wakibadilishiwa adhabu kutoka adhabu ya kunyongwa na kuwa kifungo cha maisha.
Kulingana na taarifa ya Wizara ya mambo ya ndani, msamaha huu haukuwahusu wafungwa waliohukumiwa kwa makosa ya kujamiiana, kubaka, utekaji au wizi wa watoto, kuwapa mimba wanafunzi, waliohukumiwa kwa makosa ya unyang'anyi wa kutimia silaha, waliokutwa na viungo vya binadamu na wale waliohukumiwa kwa makosa ya wizi wa fedha za serikali au na waliojihusisha na nyara za serikali na ujangili.

Social Plugin