Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTANDA AAGIZA UKAGUZI MKALI WA MAZINGIRA MWANZA


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ametoa wito kwa wananchi kushiriki ipasavyo katika kutunza Mazingira huku akilitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na maafisa mazingira wa Halmashauri kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara za kimazingira ili kuhakikisha usafi na usalama wa mazingira unaimarishwa.

Akizungumza katika kikao na viongozi wa NEMC pamoja na wanahabari, Mhe. Mtanda alisisitiza umuhimu wa utekelezaji madhubuti wa Sheria za mazingira ili kulinda rasilimali za asili na afya ya jamii.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 191, Serikali imeweka marufuku kwa shughuli zote zinazochangia uchafuzi wa mazingira, hususan katika maeneo ya vyanzo vya maji na maeneo tengefu.

Aidha, alifafanua kuwa Kifungu cha 57 cha sheria hiyo kinakataza mtu yeyote kujenga, kufanya shughuli au kutupa taka ndani ya umbali wa mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji au eneo la hifadhi, hatua inayolenga kulinda rasilimali hizo muhimu.

Mhe. Mtanda alibainisha kuwa marufuku hiyo imekuja kufuatia ongezeko la vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyohatarisha vyanzo vya maji, afya za wananchi pamoja na uendelevu wa rasilimali za asili.

Hivyo, serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha maeneo muhimu ya kimazingira yanahifadhiwa ipasavyo.

Katika kuimarisha utekelezaji huo, serikali kupitia mamlaka za mikoa na halmashauri imeongeza juhudi katika usimamizi wa mazingira, ikiwemo kulinda misitu, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuboresha miundombinu ya ukusanyaji na utupaji wa taka.

Sambamba na hilo, ukaguzi wa kimazingira unaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali yenye shughuli za kijamii na kiuchumi kama vile baa, kumbi za starehe, viwanda na maeneo ya biashara.

Lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha kuwa shughuli zote zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya usafi, usalama na utunzaji wa mazingira.

Alionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukiuka sheria za mazingira.

Hatua hizo ni pamoja na kufutiwa leseni za biashara na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria kwa wahusika wa vitendo kama utupaji taka ovyo, ujenzi holela katika vyanzo vya maji na uchomaji wa misitu.

Aidha, serikali inaendelea kushirikiana na wananchi kwa kutoa elimu ya mazingira na kuendesha kampeni za uhamasishaji ili kuongeza uelewa wa umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Ushirikiano huo umetajwa kuwa ni muhimu katika kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com