Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUJAT YASISITIZA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI, UENDANE NA UWAJIBIKAJI KWA UMMA VIJIJINI

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT), Neville Meena na Katibu wa RUJAT Prosper Kwigize (kushoto)
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT), Neville Meena

Na Kadama Malunde, Arusha

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT), Neville Meena, amesema kuwa uhuru wa vyombo vya habari unapaswa kuambatana na uwajibikaji na kuwataka waandishi wa habari kuzingatia misingi ya taaluma yao hata wanapokutana na changamoto mbalimbali.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika kitaifa April 30 jijini Arusha.

Meena alisema washiriki walikutana kujadili mustakabali wa sekta ya habari katika muktadha wa mabadiliko ya kidijitali, wakizingatia kaulimbiu ya mwaka huu inayohimiza kulinda uhuru wa habari, kukuza ubunifu na kuhakikisha uendelevu wa taaluma hiyo.

Alieleza kuwa pamoja na umhimu wa uhuru wa habari, wanahabari wanapaswa kuendelea kuzingatia kanuni za msingi za taaluma ambazo ni ukweli, usahihi, uwiano na maslahi ya umma, huku akionya kuwa utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma haupaswi kuzuiwa kwa vitisho, unyanyasaji au vikwazo vinavyokiuka haki za wanahabari.

Aidha, Meena alibainisha kuwa kwa kuzingatia maazimio ya maadhimisho ya mwaka 2026 ya World Press Freedom Day, RUJAT inatoa wito kwa Serikali kuendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa uhuru wa habari, kulinda usalama wa wanahabari na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa za umma kwa uwazi na kwa wakati.

Aliongeza kuwa sekta ya habari nayo inapaswa kubuni mifumo endelevu ya kiuchumi, kuwekeza katika ubora wa maudhui na kutumia teknolojia mpya ikiwemo akili Unde (AI) kwa manufaa ya jamii.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo aliipongeza Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kwa pendekezo la kuunda kamati ya pamoja kati ya wadau wa habari na Wizara, hatua aliyoitaja kuwa ni fursa muhimu ya kusogeza mbele hoja za kitaaluma zilizojadiliwa katika mkutano huo wa Arusha.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijini RUJAT, Bw. Prosper Kwigize, alisema chama hicho kimepata fursa ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo pamoja na kuwa sehemu ya Kamati ya Taifa ya kuratibu siku hiyo muhimu.

Kwigize alisisitiza kuwa RUJAT ni wawakilishi halali mhimu wa sauti za wananchi wa vijijini ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakiachwa nyuma katika upatikanaji wa taarifa na ushiriki katika masuala ya habari, akibainisha kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inaakisi hali halisi ya wananchi hao ambao ndio wanaoathirika zaidi wakati wa migogoro ya amani na changamoto za kiusalama.


Alieleza kuwa wakazi wa vijijini ndio huathirika zaidi pale panapotokea sintofahamu ya amani na usalama, hukosa fursa stahiki za kupata taarifa sahihi na kwa wakati. 

Aliongeza kuwa changamoto za miundombinu ya mawasiliano, uwekezaji mdogo wa vyombo vya habari vijijini pamoja na mwamko mdogo wa kuripoti habari za maeneo hayo zimeendelea kufinyanga upatikanaji wa habari kwa wananchi wa vijijini.

Kutokana na hali hiyo, alisema RUJAT imejipanga kuunganisha nguvu na taasisi mbalimbali za sekta ya habari zikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), MISA Tanzania, Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania, UNESCO, TAMWA , TADIO, na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha habari za maendeleo vijijini zinapewa kipaumbele katika vyombo vyote vya habari ndani na nje ya Tanzania kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Alisema ushirikiano huo unalenga kubadili mtazamo uliopo na kujenga mwelekeo mpya wa uandishi wa habari nchini unaojali maslahi ya umma, dira ya maendeleo ya Taifa na kutoa suluhisho la changamoto zinazolikabili jamii.

Kwigize alisisitiza kuwa lengo kuu ni kuondokana na dhana ya kuandika na kutangaza habari za mijini au zinazojali zaidi wanasiasa bila kuzingatia maoni ya jamii, na badala yake kuwekeza katika kuibua, kuandika na kusambaza habari zenye maslahi mapana ya umma, hususan kutoka maeneo ya vijijini.

Aliongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu ni chachu ya kuanzisha safari mpya ya kujenga taswira sahihi ya amani, usalama na maendeleo vijijini kupitia mawasiliano yenye tija na uandishi wa habari chanya unaogusa maisha halisi ya wananchi.

Kwa pamoja, viongozi hao wa RUJAT wamehimiza wanahabari kuimarisha mshikamano, kutetea haki zao kwa njia za kisheria na kitaaluma pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kupambana na taarifa potofu, ili kujenga sekta ya habari iliyo huru, salama, bunifu, inayoaminika na endelevu kwa maendeleo ya Taifa.

Katika maadhimisho hayo Chama cha waandishi wa Habari vijijini (RUJAT) kimewakilishwa na viongozi wa kamati tendaji kwa ufadhili wa kampuni ya MATI Foundation ya mkoani Manyara ambayo inahamasisha ushiriki wa vyombo vya habari katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa mstakabali wa uchumi wa taifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com