Na Fadhili Abdallah-Kigoma
Wataam wa afya ya uzazi wamekutana mkoani Kigoma kufanya tathmini kufuatia kuibuliwa kwa changamoto mbalimbali zinazochangia kuendelea kwa vifo vya mama wajawazito na watoto.
Kikao hicho kinafanyika ikiwa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa kunusuru vifo vya mama wajawazito na watoto unaotekelezwa na Shirika la Thamini Uhai ambapo ukaguzi uliofanywa kwenye vituo 138 vya kutoa huduma mkoani Kigoma unaonyesha kuwa jitihada zaidi zinahitajika kunusuru vifo hivyo.
Dk.Mkambu Kasanga Mshauri Mwandamizi masuala ya afya ya uzazi Shirika la Thamini Uhai
Akiwasilisha taarifa ya ukaguzi na tathmini iliyofanywa na wataalam hao Mshauri Mwandamizi wa masuala ya afya ya uzazi, Dk.Mkambu Kasanga alisema kukosekana kwa vifaa vya kuzuia mama mjamzito kutokwa na damu nyingi (PPH TRAY) katika vituo vingi vya kutoa huduma kunachangia kuendelea kwa vifo vya Mama wajawazito.
Dk.Mkambu amesema kuwa ukaguzi na tathmini walioifanya inaonyesha kuwa ni asilimia 18 ya vituo vya kutoa huduma havina hivyo vifaa huku kukiwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na uzoefu wa matibabu ya kifafa cha uzazi kwa watumishi wapya wa afya walioajiriwa hivi karibuni.
Akizungumza katika mkutano huo Mratibu wa miradi wa Shirika la Thamini Uhai, Dk.Sunday Dominico amesema kuwa wadau kwa pamoja wanahitaji kukaa pamoja na kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo kutoa mafunzo kwa watumishi wapya namna ya kuhudumia mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Dk.Sunday Dominico Mratibu wa miradi Shirika la Thamini Uhai
Victoria Lyimo mratibu wa kitengo cha Mama Mjamzito na watoto wizara ya afya.
Kwa upande Mwakilishi kutoka kitengo cha Mama na Mtoto wizara ya afya,Dk.Victoria Lyimo amesema kuwa wameiona changamoto ya uwepo wa idadi kubwa ya watumishi wa afya nchi nzima na wameandaa kitita cha kutoa mafunzo kwa watumishi wote wanaohusika na masuala ya afya ya uzazi na mafunzo hayo yataanza kutolewa mkoani Kigoma Machi tisa mwaka huu.
Mganga Mkuu wa Mkoa Kigoma,Dk.Edward amesema kuwa wamezipokea changamoto hizo na kwamba timu ya afya ya mkoa itaainisha kila mdau kwa kila ngazi na namna anavyotakiwa kukabili changamoto kiutendaji kwenye eneo lake.

Social Plugin