Na Mwandishi wetu
Wananchi wa jamii ya Kimaasai kutoka Ngorongoro wameeleza msimamo wao wa pamoja wakisisitiza kuwa ardhi yao si rasilimali ya kawaida, bali ni sehemu ya uhai, utamaduni na historia yao.
Wamesema maamuzi yote yanayohusu matumizi ya ardhi yanapaswa kuzingatia hali halisi ya maisha yao pamoja na kushirikisha kikamilifu sauti za wananchi.
Wananchi hao wameeleza kuwa wanaamini uwazi na ushirikishwaji wa kweli ni msingi wa haki, wakibainisha kuwa ripoti na mipango inayotolewa bila kuakisi uhalisia wa maisha yao huacha maswali mengi bila majibu. Wamesema hali hiyo huongeza hofu miongoni mwa jamii badala ya kuleta suluhisho la kudumu.
Pamoja na hayo, wameiombaserikali kuhakikisha unakuwepo kwa mchakato unaojali watu, unaosikiliza maoni ya wananchi na kutafuta uwiano kati ya uhifadhi wa mazingira na maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mwananchi wa Ngorongoro, Lebanguti Moso, amesema wanamuomba Mheshimiwa Rais kuangalia upya suala la ardhi hiyo ambayo ni ya mababu zao. Pia ameomba eneo la Ziwa Natroni lisiwekwe kuwa pori la akiba.
Aidha, Moso amesisitiza kuwa maeneo yanayotumika kwa malisho ya mifugo yaendelee kubaki kwa matumizi hayo, akieleza kuwa jamii hiyo inategemea ufugaji kama chanzo kikuu cha maisha yao.
Ameongeza kwa kuomba kukomeshwa kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wafugaji pamoja na mifugo yao.




Social Plugin