Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI BUZINZA WATAJA MCHANGO WA BIMA YA AFYA KUOKOA MAISHA NA KUONDOA MIGOGORO

                       Na Sumai Salum- Kishapu

Wananchi 205 wa Kijiji cha Buzinza, Kata ya Masanga, wamepokea Bima ya afya kwa watu wote kupitia mpango wa serikali unaolenga kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bila kikwazo cha gharama.


Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na wakazi wa kijiji hicho, wengi wakisema bima ya afya ni msaada mkubwa hasa kwa wananchi wa vijijini ambao mara nyingi hushindwa kumudu gharama za matibabu.


Kwa muda mrefu baadhi ya wananchi wa maeneo ya vijijini wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kuchelewa au kushindwa kabisa kwenda hospitalini kutokana na kukosa fedha za matibabu. Hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya wagonjwa kuendelea kuugua bila kupata matibabu sahihi au kutafuta tiba mbadala zisizo na uhakika wa kitaalamu.


Akizungumza kuhusu umuhimu wa bima ya afya, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bulekela, Kwalu Mantana Mahoiga, amesema mpango huo unawapa wananchi matumaini mapya ya kupata huduma za afya kwa wakati.


“Ninaishukuru sana serikali kwa kutupatia bima ya afya. Hii inatupa uhakika wa kupata matibabu hospitalini bila kuogopa gharama. Kwa wananchi wa vijijini kama sisi ambao kipato cha familia zetu ni duni, hii ni msaada mkubwa kwa sababu afya ni msingi wa maisha na maendeleo,” amesema Mantana.
Mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Bulekela Kata ya Masanga wilayani kishapu mkoani Shinyanga, Kwalu Mantana Mahoiga, akizungumzia umuhimu wa bima ya afya kwa watu wote              

                          
Ameongeza kuwa uwepo wa bima ya afya utasaidia wananchi kujenga tabia ya kuwahi hospitalini wanapopata matatizo ya kiafya badala ya kusubiri hadi hali inakuwa mbaya.


Nae Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Buzinza, Godliver Elias Mayunga amesema ukosefu wa bima ya afya umekuwa ukichangia baadhi ya wananchi kukwepa hospitali na kuishia kutegemea imani za kishirikina au matibabu yasiyo rasmi.


“Watu wengi walikuwa wanashindwa kwenda hospitali kwa sababu ya kukosa fedha. Wengine walilazimika kwenda kwa waganga wa kienyeji bila kujua tatizo halisi la afya zao. Kupitia bima ya afya, wananchi sasa wataweza kupata matibabu ya kitaalamu mapema na kuepuka madhara makubwa au vifo vinavyoweza kuzuilika,” amesema Mayunga.


Naye mkazi mwingine wa Kijiji cha Buzinza, Nyanzobe Jisinza, amesema hatua ya serikali kugawa bima hizo inaonesha dhamira ya dhati ya kuwajali wananchi hasa wale wenye kipato cha chini.

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Buzinza Kata ya Masanga wilayani kishapu mkoani Shinyanga,Godliver Elias Mayunga, akizungumzia umuhimu wa bima ya afya kwa watu wote


“Kupata bima ya afya ni kama kupata kinga ya maisha. Inatupa uhakika kwamba hata kama tutapata matatizo ya kiafya, tunaweza kwenda hospitali yoyote iwe ngazi ya Kijiji ama Taifa na kupata matibabu ya kitaalamu bila kuathiri sana hali ya kifedha ya familia,” amesema Jisinza.


Ameongeza kuwa kuna wakati jamii upoteza wapendwa wao kwa vifo na wengine kufarakana sababu ikiwa ni imani za kishirikina ambapo baadhi ya wataalamu wa tiba asili huwapa maelekezo yasiyosahihi ila upataji huduma za kitaalamu hospitali utasaidia kuondokana na hatari hizo na jamii kubakia salama.


Wananchi wa kijiji hicho wameishukuru serikali kwa mpango huo wakisema utasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kutafuta matibabu ya kitaalamu hospitalini badala ya kuchelewa au kutegemea tiba zisizo rasmi.


Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi wakati wa uzinduzi wa Bima ya afya ngazi ya wilaya mnamo Februari 27,2026 alisema jumla ya Wananchi 11, 535 walioko kwenye mpango  wa kunusuru kaya masikini (TASAF) watanufaika na mpango huo sawa na wastani wa kaya 2,257 kwa mchango wa 150,000 kwa kila kaya kwa wilayani humo huku Kijiji cha Bubinza kikawa na wanufaika 205.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kupata matibabu ya kitaalamu hospitalini kunasaidia wagonjwa kugundua magonjwa mapema, kupata ushauri sahihi wa kitabibu pamoja na dawa zinazofaa kwa ugonjwa husika. Hali hiyo huongeza uwezekano wa kupona haraka na kupunguza hatari ya madhara makubwa kwa afya.


Mpango wa kuwapatia wananchi bima ya afya unaendelea kuonekana kama hatua muhimu katika kuimarisha afya za jamii, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu kwa wakati.
Mkazi wa Kijiji cha Buzinza Kata ya Masanga wilayani kishapu mkoani Shinyanga, Nyanzobe Jisinza, akizungumzia umuhimu wa bima ya afya kwa watu wote














Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com