Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKIMBIZI WA BURUNDI WAONDOKA TANZANIA, WAKIISHUKURU SERIKALI KWA MAKAZI



Na Mwandishi wetu, Kigoma

Maelfu ya raia wa Burundi waliokuwa wakiishi kwenye Kambi ya wakimbizi ya Nduta Wilayani Kibondo na Kambi ya Nyarugusu Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wameendelea kuondoka nchini kurejea nchini Burundi, wakiishukuru serikali ya Tanzania kwa makazi na huduma zote muhimu walizokuwa wakizipata.

Wakisisitiza kuwa hawajalazimishwa ama kushinikizwa na yeyote kuondoka nchini au kunyimwa huduma muhimu za kijamii ikiwemo chakula kama shinikizo la wao kuondoka nchini, Wakimbizi hao kwa nyakati tofauti wameeleza furaha yao ya kurejea Burundi ili kushiriki katika ujenzi wa Taifa lao.

"Ninaishukuru serikali ya Tanzania kwa muda wote niliokaa hapa na ninaamini sasa naenda kuishi vizuri zaidi kwasababu nitakuwa nchini kwetu maana wanasema Mkataa kwao ni mtumwa na uzuri ni kuwa kurudi nyumbani kwetu pia ni sifa kwani kunatuondoa katika kuitwa Wakimbizi." Amesema Bw. Uwase Nshimirimana.

Aidha akizungumzia kuhusu zoezi hilo la kuondoka nchini kwa Wakimbizi hao wa Burundi, Mratibu msaidizi wa Idara ya huduma kwa wakimbizi Kanda ya Magharibi Bw. Novatus Panda amekanusha uvumi kuhusu Raia hao wa kigeni kulazimishwa kwenda makwao pamoja na kunyimwa chakula, akisema Shirika la chakula duniani WFP halijawahi kusitisha utoaji wa chakula kwa wakimbizi nchini.

Kulingana na tangazo la serikali kufikia Machi 31, 2026 Kambi ya Nduta itafungwa rasmi, huku Kambi ya Nyarugusu ikitarajiwa kufungwa mnamo Juni 2026 kwa wakimbizi kutoka nchini Burundi, tangazo likitolewa pia kwa wale wanaoondoka kwa hiari kuruhusiwa kuvunja nyumba zao na kuondoka na vifaa mbalimbali vya ujenzi katika nyumba zao ili kwenda kuwasaidia katika Taifa lao.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com