Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azzan Zungu (Mb), ametangaza kuahirishwa kwa vikao vyote vya Kamati za Kudumu za Bunge vilivyokuwa vifanyike leo, Machi 25, 2026, kutokana na maombolezo ya kifo cha Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Vangimembe Lukuvi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, uamuzi huo umefikiwa kufuatia kupokelewa kwa taarifa za msiba huo mzito ulioligusa Bunge na Taifa kwa ujumla.
Lukuvi, ambaye pia alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), amefariki dunia asubuhi ya leo Machi 25,2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Spika Zungu ameeleza kuwa kuahirishwa kwa shughuli hizo kunazingatia Kanuni ya 176 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Agosti 2025, inayoruhusu kusimamishwa kwa shughuli za Bunge katika mazingira ya maombolezo ya kitaifa au msiba wa kiongozi.
Kifo cha Mheshimiwa Lukuvi ni pigo kwa Bunge na Serikali, kikiacha pengo katika uongozi na utumishi wa umma alioutumikia kwa muda mrefu.

Social Plugin