Tanzania imeendelea kudhihirisha ukongwe na uthabiti wake katika ramani ya utalii duniani baada ya kupata mafanikio makubwa kwenye maonesho ya ITB Berlin nchini Ujerumani.
Ushiriki huu wa kihistoria, uliokutanisha nchi zaidi ya 180, ni jibu tosha kwa watu wenye hila na ubinafsi waliojaribu kupaka matope tasnia ya utalii nchini kwa maslahi yao binafsi. Licha ya jitihada za baadhi ya vikundi kutaka kuichafua tasnia hii inayobeba maisha ya mamilioni ya Watanzania, banda la Tanzania limegeuka kuwa kivutio kikuu, likithibitisha kuwa ukweli na uzuri wa nchi yetu hauwezi kufichwa kwa propaganda za chuki.
Chini ya uongozi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Wizara ya Maliasili na Utalii, zaidi ya kampuni 70 na washiriki 169 waliiwakilisha nchi kwa uzalendo wa hali ya juu.
Siku ya tatu ya maonesho hayo, iliyobatizwa jina la 'Tanzania Day', iligeuka kuwa sherehe ya kitaifa jijini Berlin, ambapo ladha ya vyakula vya asili, muziki, na ukarimu wa kipekee wa Watanzania viliwavuta mamia ya wageni na wawekezaji. Hii ni ishara kuwa ulimwengu hautazami maneno ya watu wenye nia ovu, bali unatazama ukweli wa "Destination Tanzania Unforgettable"—kitovu cha utalii barani Afrika.
Mafanikio haya ni ushindi mkubwa kwa maslahi ya taifa na maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja. Utalii unachangia sehemu kubwa ya fedha za kigeni na kutoa ajira kwa vijana wengi kuanzia waongoza watalii, madereva, hadi mama lishe.
Kwa kufungua milango mipya ya biashara nchini Ujerumani, serikali imehakikisha kuwa mipango ya kuangusha sekta hii inagonga mwamba. Tanzania imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama World Leading Safari Destination, huku ikionyesha kuwa umoja wa Watanzania katika kutangaza vivutio vyetu ni nguvu kubwa kuliko hila yoyote ya kibinafsi.
Kupitia ushiriki huu, Serikali ya Awamu ya Sita imetuma ujumbe mzito duniani: Tanzania ipo salama, inakaribisha wageni, na haitayumba katika kulinda rasilimali zake kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Kila mkataba wa uwekezaji uliosainiwa Berlin ni pigo kwa wale wanaotaka kuona utalii wetu ukishuka, na ni ushindi kwa kila Mtanzania anayefaidika na mnyororo wa thamani wa sekta hii adhimu.
Social Plugin