Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS KANDA YA ZIWA MASHARIKI YATEKETEZA BIDHAA ZISIZOFAA SOKONI

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa Mashariki limekamata na kuteketeza kiasi cha tani 3.9 cha bidhaa mbalimbali ambazo hazipaswi kuwa sokoni baada ya kuisha muda wa matumizi, zenye lugha isiyotambulika kwa watumiaji na zilizopigwa marufuku kisheria.

Zoezi la kuteketeza bidhaa hizo limefanyika Ijumaa Machi 13, 2024 katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza, likisimamiwa na Afisa Udhibiti Ubora wa TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, James James.

"Miongoni mwa bidhaa tulizoziondoa sokoni ni nguo za mitumba za ndani, nguo za kuogelea, soksi, gloves na taulo. Zilikuwa sokoni kinyume na matakwa ya viwango vya ubora ambapo kiwango namba 578 kinakataza kuingiza sokoni bidhaa hizo za mitumba" amesema James.

James ametaja bidhaa zingine zilizoondolewa kwenye stoo na masoko mbalimbali Kanda ya Ziwa Mashariki kuwa ni za chakula na vinywaji zilizotoka nje ya nchi zikiwa zimeandikwa kwa lugha isiyo ya Kiswahili ama Kiingereza kwa kuwa mlaji hawezi kuelewa uhalali ama ukomo wa matumizi ya bidhaa hizo.

"Pia tumeondoa bidhaa za vipodozi ambazo zimeisha muda wa matumizi ambapo zoezi hili linalenga kulinda usalama na afya ya mtumiaji. Tunaendelea kutoa rai kwa wananchi kukagua bidhaa kabla ya kununua. Bidhaa nyingine zinaweza kuwa halali sokoni, lakini kama zimeisha muda wa matumizi zinaweza kugeuka sumu kwa mtumiaji" amesisitiza James.

Aidha James amewahimiza wafanyabiashara kufuata sheria na taratibu kabla ya kuingiza bidhaa sokoni ili kuepuka faini ya uteketezaji pindi wanapokutwa nazo ambapo amebainisha kuwa TBS imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kwa wananchi na wafanyabiashara ili kuzitambua hivyo ni vyema wakazingatia elimu hiyo.

Nao baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza akiwemo Haibary James na Maria Peter wametaka TBS kuendelea kukagua na kuondoa sokoni bidhaa zote zisizokidhi viwango ili kuwalinda watumiaji huku wakisisitiza wananchi kuwa utaratibu wa kukagua bidhaa kabla ya kununua.
Na George Binagi, Mwanza
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, James James (kushoto) akisimamia zoezi la uteketezaji wa bidhaa zilizoondolewa sokoni kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa Mashariki.
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, James James akionyesha nguo mbalimbali za mitumba ikiwemo taulo ambazo zimetekezwa.
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, James James akionyesha bidhaa za vipodozi zilizoteketezwa. 
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, James James akionyesha bidhaa za chakula zilizoteketezwa.
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, James James akisimamia zoezi la uteketezaji wa bidhaa mbalimbali zisizofaa kwa matumizi.
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, James James akieleza kuhusu bidhaa mbalimbali ikiwemo za nguo, chakula na vipodozi zilizokamatwa na kuondolewa sokoni na TBS Kanda ya Ziwa Mashariki.
Mkazi wa Kata ya Buhongwa jijini Mwanza, Haibary James akizungumza na wanahabari na kutoa pongezi kwa TBS Kanda ya Ziwa Mashariki baada ya kushuhudia zoezi la kuteketeza bidhaa zisizofaa kuwa sokoni.
Mkazi wa Kata ya Buhongwa jijini Mwanza, Maria Peter akizungumza na wanahabari na kutoa pongezi kwa TBS Kanda ya Ziwa Mashariki baada ya kushuhudia zoezi la kuteketeza bidhaa zisizofaa kuwa sokoni.
Bidhaa mbalimbali ikiwemo za nguo, chakula na vipodozi zikiteketezwa baada ya kuondolewa sokono na TBS Kanda ya Ziwa Mashariki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com