Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA SIASA YA CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YASISITIZA UTEKELEZAJI SAHIHI WA ILANI YA CCM



Katibu wa siasa, itikadi na uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Said Bwanga akisoma taarifa hiyo leo Ijumaa Machi 13, 2026.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini imewasilisha mapendekezo yake kufuatia kupokea na kujadili taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2025–2030 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, kwa mujibu wa Ibara ya 75 (3) na Ibara ya 76 (4) ya Katiba ya CCM Toleo la Mei 2025.

Taarifa hiyo imesomwa na katibu wa siasa, itikadi na uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Said Bwanga na kwamba kikao hicho kimepokea, kujadili na kutoa ushauri, maelekezo pamoja na maagizo kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Chama, sambamba na kusimamia utekelezaji wa siasa na maelekezo ya chama kwa ujumla.

Katika hatua hiyo, Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya baada ya kupokea taarifa ya Serikali iliyowasilishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, iliijadili kwa kina na kisha kutoa mapendekezo mbalimbali kwa kuzingatia utekelezaji wa miradi na maendeleo ya sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa tathmini ya Kamati ya Siasa, imebainika kuwa miradi mingi iliyotekelezwa katika kipindi hicho imefanikiwa kutokana na fedha zilizotolewa na Serikali Kuu kupitia Hazina, michango ya wafadhili pamoja na nguvu za wananchi.

Taarifa hiyo pia imeonyesha kuwa bajeti ya Halmashauri katika utekelezaji wa maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ilikuwa jumla ya shilingi 42,285,083,200. Kati ya fedha hizo, mapato ya ndani yalikuwa shilingi 7,463,922,000, ruzuku ya uendeshaji wa ofisi shilingi 2,007,013,000, miradi ya maendeleo kupitia ruzuku ya Serikali Kuu na wahisani shilingi 9,215,299,000, huku ruzuku ya mishahara ikiwa shilingi 23,597,949,200.

Hadi kufikia Desemba 2025, jumla ya shilingi 17,877,245,861.78 zilikuwa zimetumika, sawa na asilimia 92 ya mapato yote yaliyokusudiwa kutumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Baada ya kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali, Kamati ya Siasa imebaini kuwa miradi mingi iliyotekelezwa imefikia hatua nzuri huku michache iliyobaki ikiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji. Kutokana na hali hiyo, Kamati imehimiza juhudi zaidi ziwekwe ili kukamilisha miradi yote iliyopangwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Hivyo, Kamati ya Siasa ya Wilaya imependekeza kuwa Halmashauri isianzishe miradi mipya wakati bado kuna miradi ambayo haijakamilika, pamoja na Serikali kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Katika sekta ya Kilimo na Mifugo, Kamati imependekeza Serikali iendelee kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji kuhusu mbinu bora za kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Aidha, katika eneo la mifugo na uvuvi, Serikali imeshauriwa kuwahimiza na kuwaelekeza Maafisa Ugani wa Kata kufanya kazi kwa karibu na wananchi katika kuwasaidia kupata kinga na mbinu bora za kudhibiti magonjwa ya mifugo. Serikali pia inashauriwa kuendelea kuunda vikundi vya SACCOs kwa wafugaji na kuvipa kipaumbele katika shughuli za kununua na kuuza mifugo kwa wanunuzi au viwanda ili kulinda bei ya soko la ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Kwa upande wa sekta ya miundombinu, Kamati imependekeza Serikali ya Wilaya kuchukua hatua za kuhamasisha wananchi wengi zaidi kupata hati miliki za viwanja vyao, kwani utekelezaji wa utoaji wa hati kwa sasa haujafikia kiwango kinachoridhisha. Pia imependekezwa kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma hizo ili kuondoa malalamiko ya wananchi.

Vilevile Serikali imeshauriwa kuendelea kupima viwanja na kuwapatia waombaji bila urasimu, pamoja na kulipa fidia kwa viwanja vinavyodaiwa ili kumaliza migogoro ya ardhi katika Manispaa. Serikali pia inapaswa kuhakikisha wananchi wanapewa viwanja vyenye namba sahihi, badala ya kuonyeshwa viwanja kisha kuambiwa namba zitatafutwa baadaye.

Katika zoezi la ugawaji wa viwanja, Kamati imependekeza Serikali kuweka kipaumbele kwa wananchi wanaodai viwanja, pamoja na kuwashirikisha wananchi katika kupata gharama za upimaji wa viwanja katika maeneo wanayoishi ili kurahisisha mchakato huo.

Kwa upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia sekta ya maendeleo ya jamii, Kamati imependekeza Serikali kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii wa Bima za Afya. Pia imeelekezwa kuhakikisha huduma za dawa kwa wazee katika Hospitali ya Wilaya zinatolewa bila usumbufu.

Kamati pia imeeleza kuwepo kwa changamoto ya matumizi ya kauli zisizo na staha kwa baadhi ya wananchi wanaoomba mikopo ya vikundi, hali inayokatisha tamaa wanavikundi. Hivyo, Serikali inapaswa kuweka usimamizi wa karibu kwa vikundi vilivyoundwa, kufuatilia urejeshaji wa mikopo na kutoa ushauri ili kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa ipasavyo.

Serikali Kuu pia imeshauriwa kufuatilia na kujiridhisha kuhusu uhalali na usahihi wa vikundi vilivyopata mikopo katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika sekta ya fedha na biashara, hususan Soko Kuu la Shinyanga, Kamati imeipongeza Serikali kwa juhudi za kuongeza vyanzo vya mapato na kuweka kodi zinazoendana na hali ya soko la sasa. Hata hivyo, imependekeza hatua zaidi zichukuliwe ili kuongeza mapato ya ndani na kuimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato.

Pia Serikali imeshauriwa kuendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kuhusu namna bora ya kuandaa na kufungasha bidhaa za nafaka. Aidha, Kamati imebaini kuwa kibanda cha mfano kilichojengwa katika soko kuu hakikidhi mahitaji ya wafanyabiashara kutokana na gharama kubwa za ujenzi na muundo wake kutokidhi matumizi yaliyokusudiwa, hali iliyosababisha wafanyabiashara kukikataa.

Katika sekta ya huduma za jamii, Kamati imeelekeza Serikali kusimamia kwa karibu changamoto zinazojitokeza katika shule za msingi, ikiwemo ujenzi wa vyoo na madarasa. Serikali pia imepongezwa kwa kujenga miundombinu ya shule za msingi Bugayambebele, Mwenge, Kizumbi na Mwanase iliyopo Kolandoto.

Kwa upande wa shule za sekondari, Serikali imeelekezwa kutoa taarifa bayana kuhusu hali ya ufaulu wa wanafunzi waliojiunga na sekondari ili kubaini kama kuna ongezeko la ufaulu au la, jambo litakalosaidia kupima mafanikio yaliyofikiwa.

Vilevile Serikali inatakiwa kushughulikia upatikanaji wa walimu wa masomo ya sayansi ili kuondoa upungufu uliopo. Aidha, Serikali ya Wilaya inapaswa kusimamia kwa karibu ujenzi wa madarasa unaoendelea ili kujiridhisha na gharama halisi za ujenzi pamoja na kuchunguza gharama za ujenzi wa madarasa na ofisi za walimu.

Katika sekta ya afya, Serikali imeelekezwa kufuatilia ujenzi wa Zahanati ya Mwanibu. Pia Serikali ya Wilaya imeshauriwa kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu matumizi ya kauli zisizo na staha kutoka kwa baadhi ya wahudumu wa Hospitali ya Wilaya.

Kwa upande wa idara ya maji, Kamati imebainisha kuwa mradi wa huduma ya maji Kolandoto unaendelea vizuri, lakini imeishauri Serikali kuongeza kasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati. Serikali pia imeshauriwa kusimamia kwa karibu usambazaji wa huduma ya maji, hususan katika maeneo ya vijijini.

Katika sekta ya ujenzi wa barabara, Kamati ya Siasa imeeleza kutoridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Nguzo Nane hadi Mwawaza, kwani mradi huo umechelewa kukamilika na kuwasababishia wananchi usumbufu. Hivyo Serikali imeelekezwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo.

Vilevile Kamati haijaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa stand ya Mkoa wa Shinyanga, ambapo imeelezwa kuwa mradi huo uko nje ya muda uliopangwa na kuna malalamiko ya vibarua kutolipwa kwa wakati pamoja na kutokuzingatiwa kwa baadhi ya taratibu za utekelezaji wa miradi mikubwa. Kutokana na hali hiyo, Kamati imeielekeza Serikali kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo.

Kamati ya Siasa imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiletea Wilaya miradi mingi ya maendeleo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza maendeleo na kuifanya kuwa miongoni mwa wilaya zinazoendelea kwa kasi nchini.

Pia Kamati imeipongeza Serikali ya Mkoa na Wilaya kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, kwa mchango wake katika maendeleo ya Wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amesema amepokea maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuyasimamia ipasavyo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.



Amesema Serikali ya Wilaya ya Shinyanga itaongeza nguvu katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ile iliyoelezwa kuwa na changamoto, sambamba na kuhakikisha maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Siasa yanatekelezwa kwa wakati kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi. Katibu wa siasa, itikadi na uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Said Bwanga akisoma taarifa hiyo leo Ijumaa Machi 13, 2026.Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza.

Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.



Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.



Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.




Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.




Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.




Viongozi mbalimbali.




Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Mhe. Anord Makombe, akiandika maoni, mapendekezo na maswali mbalimbali yanayoulizwa na wajumbe.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Salum Kitumbo.


Viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.





Kikao kikiendelea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com