Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANESCO KUANZA KUKAGUA MIUNDOMBINU YA UMEME KWA NDEGE NYUKI


.Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia baada ya kuzindua rasmi matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) kwa ajili ya kukagua miundombinu yake ya kusafirisha na kusambaza umeme nchini.

Hatua hiyo inalenga kuleta mapinduzi katika utendaji kazi kwa kuongeza ufanisi na kupunguza muda unaotumika kubaini hitilafu zinazosababisha kukatika kwa nishati hiyo muhimu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika ofisi za TANESCO Ubungo, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Lazaro Twange, amebainisha kuwa teknolojia hiyo ni mwarobaini wa changamoto za kijiografia.

Kwa sasa, TANESCO inasimamia mtandao mpana wenye njia za kusafirisha umeme zenye urefu wa kilometa 8,500 na njia za kusambaza zinazofikia takribani kilomita 200,000, ambazo nyingi hupita katika maeneo magumu kama mapori na milima.

Twange amefafanua kuwa drones hizo zitasaidia shirika hilo kufanya ufuatiliaji wa karibu wa miundombinu hiyo bila kuhitaji wafanyakazi kutembea umbali mrefu au kupanda nguzo katika maeneo hatarishi. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa huduma ya umeme inarejea kwa haraka pindi changamoto zinapojitokeza, hivyo kupunguza usumbufu kwa wateja na kuimarisha uchumi wa nchi unaotegemea nishati hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kibamba, Salma Yahaya, ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yataondoa ugumu wa kufika katika baadhi ya maeneo wakati wa ukaguzi, hususan nyakati za mvua au katika maeneo yenye uoto wa asili uliokithiri.

Drones hizo zina uwezo wa kutoa picha za haraka na za uhakika zinazowawezesha mafundi kujua mahali halisi palipo na tatizo na kwenda kufanya matengenezo kwa usahihi.

Uwekezaji huu wa TANESCO unatajwa kuwa ni sehemu ya mikakati ya shirika hilo kujigeuza kuwa la kidijitali zaidi ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani. Wananchi wanatarajia kuona mabadiliko chanya katika upatikanaji wa umeme wa uhakika, huku shirika likipunguza gharama za uendeshaji na kuongeza usalama wa wafanyakazi wake wanapokuwa kazini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com