Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

e-UTATUZI: MKOMBOZI WA KASI KATIKA KUKABILI MIGOGORO YA KAZI TANZANIA



Safari ya mageuzi ya kidijitali nchini Tanzania imepiga hatua nyingine kubwa kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA). Katika kile kinachoonekana kuwa ni mapinduzi ya utoaji haki, mfumo mpya wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri, e-Utatuzi, umeanza kung’ara kwa kasi ya ajabu ndani ya muda mfupi tangu kuzinduliwa kwake.

Ndani ya kipindi cha siku 40 tu tangu kuanza kutumika kwake, mfumo wa e-Utatuzi umeweza kusajili jumla ya migogoro 663. Idadi hii ni kubwa na ya kihistoria kulinganisha na mfumo wa awali wa makaratasi, ambapo malalamiko hayakuzidi 300 kwa mwaka mzima.

Ufanisi wa mfumo huu haishii kwenye usajili tu; asilimia 40% ya migogoro yote iliyosajiliwa imeshafanyiwa maamuzi au kuhitimishwa, jambo linaloashiria mwisho wa zama za kusubiri haki kwa miaka nenda rudi.

"Mfumo huu ni kielelezo cha namna teknolojia inavyoweza kuchochea uchumi kwa kuruhusu watu kutumia muda mwingi katika uzalishaji badala ya kusubiri milolongo ya kesi," alieleza Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla.

Hayo yamebainishwa Machi 18, 2026, wakati wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii walipofanya ziara ya kikazi katika makao makuu ya Tume hiyo jijini Dar es Salaam.

Mfumo huu uliozinduliwa Januari mwaka huu, umechochewa na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kupitia uwekezaji huu, vikwazo vya kijiografia na urasimu uliokuwa ukichelewesha upatikanaji wa haki vimeondolewa, huku mlundikano wa kesi ukipungua kutoka 20,000 hadi kufikia 7,000 pekee.

Moja ya sifa kuu za e-Utatuzi ni uwezo wake wa kupunguza mianya ya rushwa. Kwa kuondoa "mtu wa kati," mashine sasa ndizo zinazochakata na kugawa mashauri kwa wasuluhishi kulingana na wingi wa kazi walizonazo (workload). Hii imeongeza uwazi na imani ya wananchi kwa Tume.

Uti wa mgongo wa mradi huu (Mradi namba 5505) ni ushirikiano wa kimfumo (Integration). e-Utatuzi umeunganishwa na mifumo mingine muhimu kama:NIDA & RITA (Uhakiki wa utambulisho),Ofisi ya Kamishna wa Kazi,e-PERMIT na Mahakama Kuu

Hatua hii inahakikisha taarifa za walalamikaji zinahakikiwa kwa sekunde chache, huku ikirahisisha ufuatiliaji wa mikataba ya kazi na kuokoa gharama za usafiri kwa wafanyakazi wa kipato cha chini.

Pamoja na mafanikio hayo, ripoti ya CMA imetaja sekta tatu ambazo bado ni "kichwa cha mwendawazimu" kwa migogoro ya kazi:Maeneo hayo ni sekta ya ujenzi,sekta ya ulinzi binafsi na sekta ya mahoteli


Aina ya migogoro inayozitesa sekta hizi ni pamoja na kuachishwa kazi bila taratibu, kuvunjiwa mikataba, na malimbikizo ya mishahara.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Rahma Riyadh Kisuo, amesisitiza kuwa serikali sasa inahama kutoka kwenye "kutatua migogoro" na kuingia kwenye kampeni ya "kuzuia migogoro" (Prevention).


Ili kufanikisha hili, serikali imeongeza ikama ya watumishi wa Tume kutoka wafanyakazi 81 hadi kufikia 200. Aidha, mfumo huu uliotengenezwa na wataalamu wazalendo wa e-GA, umezingatia usalama wa hali ya juu wa data na faragha.


Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Hawa Mchafu, ameishauri serikali kuhakikisha:Bajeti: CMA ipatiwe 100% ya bajeti iliyoombwa kwa mwaka 2025/2026 inatolewa yote kukamirisha mradi huo na Usalama wa Mtandao: Watumishi wapewe mafunzo ya ndani na nje ya nchi kupambana na wahalifu wa kidijitali (hackers).


e-Utatuzi umeweka msingi imara wa haki na usawa mahali pa kazi. Ni mapinduzi yanayoisogeza Tanzania katika ramani ya nchi zinazotumia teknolojia kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji. Haki sasa haipatikani tena kwa vumbi la barabarani, bali kiganjani mwako

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com