Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAFUNGUA MILANGO YA UTAJIRI KWA VIJANA: VIFARANGA MILIONI 10 KUZALISHWA KILA MWEZI

KATIKA mkakati kabambe wa kutatua changamoto ya ajira na kukuza uchumi wa buluu, Serikali imetangaza mpango mkakati wa kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki hadi kufikia milioni 10 kwa mwezi, hatua inayolenga kuwapa vijana nchi nzima fursa ya kuanza ufugaji wa kisasa wa viumbe maji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, akizungumza jijini Dodoma Machi 5, 2026, ametoa agizo hilo kwa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), akisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuifanya sekta ya uvuvi kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa vijana. 

Alibainisha kuwa ongezeko hili la uzalishaji kutoka kiwango cha sasa ni sehemu ya maelekezo ya Serikali kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa kutosha wa mbegu za samaki kwa gharama nafuu kwa wafugaji wadogo na wakubwa.

Waziri Kamani amefafanua kuwa Serikali inatumia programu maarufu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika sekta ya uvuvi kama injini ya kuwabadilisha vijana kuwa wajasiriamali mahiri. Kupitia programu hiyo, vijana hawatapatiwa tu vifaranga, bali watapewa mafunzo ya vitendo na mbinu za kisasa za ufugaji zinazohakikisha tija na faida ya haraka, jambo litakalowawezesha kujiajiri na kuongeza mchango wao katika Pato la Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Agness Meena, amesema Wizara imejipanga kusimamia mafunzo hayo kupitia FETA ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi stahiki. 

Alisisitiza kuwa mazingira ya amani na utulivu yaliyopo nchini yanatoa fursa ya kipekee kwa vijana kujiwekea mipango ya maendeleo, kuweka akiba, na kuwekeza kwenye miradi ya uvuvi ambayo sasa imekuwa rahisi kutokana na uwezeshaji huu mkubwa wa Serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com