Na WMJJWM Dar Es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema kuanzishwa kwa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Basket Fund - NBF) kutarahisisha upatikanaji wa rasilimali fedha na uendelevu kwa Mashirika hayo nchini.
Akizungumza Machi 18, 2026, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kwanza cha Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mchakato wa Uanzishwaji wa Mfuko huo, kilichofanyika katika ukumbi wa Four Points by Sheraton Jijini Dar es Salaam, Dkt. Jingu amesema Mfuko huo utakuwa chombo muhimu cha kuimarisha sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Dkt. Jingu ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto za utegemezi wa ufadhili kutoka nje ya nchi, ambao wakati mwingine huambatana na masharti magumu yasiyoendana na maadili na utamaduni wa Kitanzania.
“Jukumu la Mfuko huu litakuwa ni kutafuta rasilimali fedha, kuratibu utoaji wa ruzuku na kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora na kuchangia ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Dkt Jingu.
Aidha, amebainisha kuwa kutokana na mabadiliko ya sera za ufadhili kimataifa, ni muhimu kwa Mashirika hayo kubadilika na kujiimarisha kwa kutumia mikakati mbadala itakayohakikisha uendelevu wa shughuli zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Abdulmajid Nsekela, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB amesema mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yanategemea uwajibikaji wa kila mmoja kwa nafasi yake huku akisisitiza kuwa ni muhimu Wajumbe wa Kamati kufanya kazi kwa weledi, kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NacoNGO), Jasper Makala, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, amesema Mashirika mengi kwa sasa yanafanya kazi bila uhakika wa uendelevu wa miradi yao hivyo uwepo wa Kamati hiyo itasaidia kuongeza uhakika wa rasilimali fedha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumuwa Mashirika hayo.
“Mfuko huu utakuwa suluhisho muhimu kwa changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha na utasaidia Mashirika kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi zaidi,” amesisitiza Makala.
Naye Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara hiyo, ambaye pia ni Katibu wa Kamati hiyo, Vikness Mayao, amesema Mfuko huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa Mashirika hayo, kwa kuwa utaongeza tija katika utekelezaji wa miradi ya kijamii.
Ameongeza kuwa kupitia Mfuko huo, Mashirika yatapata fursa ya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.



Social Plugin