Na Bora Mustafa, Arusha.
Kongamano la Idhaa ya Kiswahili kwa vyombo vya habari duniani limefunguliwa rasmi Machi 24, 2026 katika ukumbi wa AICC jijini Arusha, likiwa na lengo la kuangazia nafasi ya lugha ya Kiswahili katika maendeleo ya kiuchumi na kidijitali.
Kongamano hilo litakaloendelea hadi Machi 27,2026 limewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari, wataalamu wa lugha pamoja na wabunifu wa masuala ya kidijitali, ambapo kwa pamoja wanajadili namna Kiswahili kinavyoweza kutumika kama nyenzo muhimu ya mawasiliano ya kimataifa.
Pia, mkutano huo unalenga kuimarisha matumizi sahihi ya Kiswahili katika sekta ya habari.
Akizungumza ,Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Amesema matumizi sahihi ya lugha hiyo yatasaidia kulinda hadhi yake na kuifanya kuwa chombo madhubuti cha maendeleo ya jamii.
Aidha, ameeleza kuwa Kiswahili kina mchango mkubwa katika uchumi, hasa katika kurahisisha mawasiliano ya kibiashara ndani na nje ya mipaka ya Afrika. Hivyo, amehimiza wadau kuendelea kukiendeleza ili kiendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa na Utamaduni, Paul Makonda, amebainisha kuwa hatua ya UNESCO kutambua Kiswahili kimataifa ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
Pia, amehamasisha taasisi mbalimbali kuanza kutumia Kiswahili kama lugha rasmi katika mikutano na majadiliano ya kimataifa.
Vilevile, vijana wametakiwa kutumia fursa zilizopo katika teknolojia ya kidijitali kukuza Kiswahili kwa ubunifu, ili kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kuwa hai na yenye ushindani katika dunia ya sasa.
.jpeg)








Social Plugin