Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FANYENI KAZI KWA BIDII, UPENDO NA USHIRIKIANO KUBORESHA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI - PROF. SHEMDOE


Na OWM – TAMISEMI, Dodoma 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM– TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewataka watumishi wa OWM- TAMISEMI kufanya kazi kwa bidii, upendo, ushirikiano, pamoja na ubunifu katika utendaji wao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Prof. Shemdoe ametoa wito huo jana Machi 26, 2026 wakati  akifungua 
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa OWM– TAMISEMI uliofanyika  Jijini Dodoma.

Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa baraza hilo litumike kama jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano miongoni mwa watumishi na kuleta ushirikiano kati ya menejimenti na wafanyakazi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

“Baraza hili lina nafasi kubwa ya kukuza upendo na ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi zetu za kila siku,” amesema Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kwa mujibu wa sheria kwa lengo la kushughulikia masuala ya msingi mahali pa kazi, ikiwa ni pamoja na utatuzi wa migogoro, maslahi ya watumishi, na kuboresha mazingira ya kazi. Aidha, amewataka watumishi kuzingatia haki, wajibu pamoja na maadili ya Utumishi wa Umma.

Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe amewahimiza wajumbe wa baraza hilo kujadili kwa kina mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 kwa kuzingatia vipaumbele vya taasisi, akisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa utekelezaji wake ni nguzo muhimu ya kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Sinyamule, amesema mabaraza ya wafanyakazi yameendelea kuwa kiunganishi muhimu kati ya uongozi na watumishi, huku akiwapongeza wajumbe kwa juhudi zao katika kuboresha utendaji kazi.

Awali, akitoa neno la utangulizi, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa OWM- TAMISEMI, Bw. Adolf Nduguru amesema mabaraza ya wafanyakazi ni vyombo vya kisheria vinavyolenga kuongeza tija, uwajibikaji, na kutoa fursa kwa watumishi kujadili masuala muhimu yanayohusu utendaji wao pamoja na maslahi yao.

Naye, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo Bw. Elias Mabele, amesema anayo imani kubwa kuwa baraza hilo litafanya kazi ya kuboresha bajeti ya OWM- TAMISEMI pamoja na Tasisi zake ili kupeleka tabasamu kwa wananchi hususan katika sekta zinazosimamiwa na Ofisi ya OWM-TAMISEMI kama Elimu, Afya, Miundombinu pamoja na Utawala Bora.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com