Na Sumai Salum - Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter N. Masindi, amezindua rasmi mafunzo kwa wawezeshaji wa stadi za maisha kupitia programu ya Dunia Yangu Bora inayotekelezwa na shirika la CAMFED mkoani Shinyanga.
Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 6, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha VETA wilayani Kishapu, ambapo Mhe. Masindi amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa wanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza na pili, ambao ndio walengwa wa kupata elimu ya stadi za maisha ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za ukuaji na maendeleo yao.
Amesema kuwa wawezeshaji hao wamechaguliwa kwa makusudi ili kuwajengea msingi imara wanafunzi mapema kabla hawajakumbana na vishawishi vinavyoweza kuathiri masomo yao.
“Sababu ya kuchaguliwa kuwa walimu na mabalozi kwa wanafunzi hawa ni kwa kuwa tunaamini mwanafunzi huanza kukutana na vishawishi vingi kuanzia kidato cha tatu na kuendelea. Kama hatakuwa amewekewa msingi imara wa kujisimamia, atashindwa kukabiliana na changamoto kama kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo pamoja na changamoto za kiuchumi za kifamilia,” amesema Mhe. Masindi.
Aidha, amewataka wawezeshaji hao kupitia programu ya Dunia Yangu Bora kuwafundisha wasichana umuhimu wa kushirikiana katika masuala mbalimbali ya maisha ikiwemo elimu, mapishi, shughuli za kilimo kupitia kanuni 10 za programu hiyo, pamoja na kujali usafi wa miili yao na mazingira yanayowazunguka na kuthamini miili yao.
“Nendeni mkawatie moyo kuwa dunia inamhitaji mwanamke msomi kwa kuwa ana nafasi kubwa katika kubadilisha jamii. Watie moyo wafikie ndoto na malengo yao. Pia ninyi wavulana muwasaidie mabinti na siyo kuwarubuni na kuwapotezea mwelekeo wa maisha,” amesisitiza Masindi.
Vilevile, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka vijana kuepuka kuishi kwa malalamiko kuhusu hali ya uchumi, badala yake wajitume kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kubadilisha maisha yao na kuondokana na utegemezi.
Kwa upande wake, Mratibu wa CAMFED Shinyanga, Suzan John, amesema kuwa shirika hilo linajihusisha na kusaidia mabinti wanaotoka katika mazingira magumu, na kupitia programu ya Dunia Yangu Bora wanaamini wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuwajenga mabinti wanaojiamini na wanaojisimamia.
“Tunaamini kuwa kupitia mafunzo haya ya siku tano, ambayo yanatarajiwa kuhitimishwa siku ya Jumanne, yatawasaidia mabinti kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo na hivyo kuendelea na masomo yao hadi kufikia ndoto zao. Pia huwa tunaendelea kuwasaidia mabinti waliomaliza kidato cha nne wanaosubiri kujiunga na kidato cha tano au vyuo,” amesema Suzan John.
Afisa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, Halmashauri ya Wilaya ya kishapu Moshi B. Moshi amesema kupitia mafunzo hayo, vijana wanajengewa uwezo wa kujitambua, kufanya maamuzi sahihi, kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuathiri mustakabali wao pamoja na kujenga misingi ya kujitegemea kiuchumi.
Programu hiyo ilitambulishwa rasmi Machi 5, 2026 katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Inalenga kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike na wa kiume kuanzia kidato cha tatu na kuendelea kutoka tarafa za Kishapu, Mondo na Negezi ili waweze kuwasaidia wanafunzi wa kidato cha kwanza na pili.
Lengo ni kuwajengea uwezo wanafunzi hao kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili, hususan vishawishi vya kimapenzi na changamoto za kiuchumi ambazo zimekuwa zikichangia baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo.
Social Plugin