Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAGANGA TIBA ASILI WATAKIWA KUZINGATIA USALAMA NA UBORA WA DAWA

Na Theophilida Felician – Geita

Waganga wa tiba asili na tiba mbadala wametakiwa kuzingatia usalama na ubora wa dawa wanazozitoa ili kulinda afya za wananchi na kuongeza ufanisi wa huduma zao.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Bi. Lucy Bed, wakati akifungua mafunzo maalum kwa waganga wa tiba asili yaliyofanyika Machi 23, 2026 mkoani Geita.

Amesema kuwa endapo viwango vya ubora na usalama vitazingatiwa, tiba asili itaendelea kuwa na mchango chanya kwa jamii, sambamba na miongozo ya Serikali kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Bi. Lucy amesisitiza kuwa utoaji wa tiba usiozingatia viwango unaweza kusababisha madhara kwa wananchi, hivyo waganga wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika utoaji wa huduma hiyo.

Aidha, ameeleza kuwa tiba asili ni urithi muhimu wa muda mrefu unaopaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa, huku akipinga vikali vitendo vya ramli chonganishi vinavyoichafua sekta hiyo. Amewataka waganga kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo hivyo ili kulinda heshima ya taaluma yao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania, Bw. Lukas Joseph Mlipu, ameainisha changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuiomba Serikali kuwatambua zaidi waganga wa tiba asili na kuwashirikisha katika masuala mbalimbali ya afya kama ilivyo kwa kada nyingine.

Amesema chama hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wanachama wake ili kuwajengea uwezo, ujuzi na weledi katika utoaji wa huduma bora kwa jamii.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali yamewakutanisha waganga kutoka mikoa ya Geita, Kagera na Shinyanga, yakilenga kuimarisha taaluma ya tiba asili na kuhakikisha inatoa huduma salama na yenye tija kwa wananchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com