
Na Paschazia Charles - Shinyanga
Wazazi na walezi katika Mkoa wa Shinyanga wamehimizwa kuhakikisha watoto wote wanaostahili kupata chanjo ya matone ya polio wanapatiwa huduma hiyo ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa polio.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo uliofanyika katika Shule ya Msingi Mapinduzi B, Manispaa ya Shinyanga, Katibu Tawala wa Mkoa huo, CP Salum Hamdun, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, amesema chanjo hiyo ni muhimu kwa afya ya watoto na inalenga kuwafikia jumla ya watoto 781,186 katika halmashauri zote za mkoa huo.
Amesema zoezi hilo litafanyika kwa njia ya nyumba kwa nyumba, mashuleni pamoja na katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa kwa urahisi.
“Chanjo hii ni muhimu kwa watoto wetu, na yeyote atakayejaribu kukwamisha zoezi hili hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesisitiza CP Hamdun.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Lucas Ndungile, amesema chanjo hiyo inalenga watoto wenye umri chini ya miaka kumi na itatekelezwa kuanzia Machi 24 hadi Machi 27, 2026, huku timu za wataalamu 1,400 zikiwa zimeandaliwa kusimamia zoezi hilo.
Naye mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi. Dinah Atinda, ambaye pia ni Mratibu wa Miradi ya Afya ya Uzazi na Mtoto, amewashukuru wazazi kwa kujitokeza kwa wingi na kuwapatia watoto wao chanjo hiyo.
Amesema zoezi hilo litafanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inaanza Machi 24 hadi Machi 27, 2026, na awamu ya pili itafanyika Mei 7 hadi Mei 10, 2026.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Shinyanga Bwana. Salum Kitumbo amewahakikishia wazazi kuwa chanjo hiyo ni salama, akiwataka kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo ili kujikinga na ugonjwa wa polio.
Amesema kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya, manispaa hiyo imejipanga kuhakikisha zoezi linafanikiwa na malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Diwani wa Viti Maalum wa Kata ya Ngokolo Bi.Veronika Massawe pia ameishukuru serikali kwa kuleta chanjo hiyo, akiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha walengwa wote wanafikiwa.
Baadhi ya wazazi na walezi waliohudhuria uzinduzi huo wameishukuru serikali kwa kuwapatia chanjo hiyo muhimu, wakiahidi kuhakikisha watoto wao wote wanapata huduma hiyo kwa ajili ya kulinda afya zao.
Chanjo ya polio inatolewa kwa watoto chini ya miaka kumi katika mikoa saba ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Geita, Simiyu, Tabora, Shinyanga na Singida, ambapo uzinduzi wa kitaifa umefanyika mkoani Mwanza ukiongozwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
























































Social Plugin