
Na Hadija Omary Mazezele
Katika msimu uliopita wa kilimo, makundi haya yalijaribu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa pamoja na mbegu zinazohimili ukame na kukomaa haraka, hatua iliyozalisha mafanikio kwa baadhi yao lakini pia kufichua changamoto kubwa.
Katika mjadala wa COP30, nchi zinazoendelea zimekuwa zikisisitiza umuhimu wa kuwalenga wakulima wadogo hasa wanawake na vijana kama nguzo ya kukabiliana na tabianchi (adaptation) na kulinda usalama wa chakula. Hali ya Tabora, inayokumbwa na mvua zisizotabirika na vipindi virefu vya ukame, imekuwa mfano halisi wa changamoto hizo.
Mafanikio:
Katika wilaya mbalimbali za Tabora, wanawake na vijana waliopata fursa ya kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kupitia maafisa ugani, redio za kijamii na simu za mkononi waliweza kupanga vizuri msimu wa upandaji. Wengi wao walichelewesha kupanda hadi mvua zilipoonekana kuwa na uhakika, hatua iliyopunguza hasara ya mbegu kukauka mapema.
Aidha, matumizi ya mbegu za mahindi na mpunga zinazostahimili ukame na kukomaa haraka yaliwasaidia wakulima kuvuna hata pale mvua zilipokatika ghafla.
Wanawake wengi walifanikiwa kupata mavuno ya kutosha kwa matumizi ya familia na ziada kidogo ya kuuza, hali iliyoongeza usalama wa chakula majumbani.
Miongoni mwa wanawake wanaojivunia mafanikio hayo ni Regina Mohamedi na Sada Masoudi,wakulima kutoka kijiji cha Chang’ombe manispaa ya Tabora ambao wanasema mbegu za kisasa zimekuwa mkombozi katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumza kuhusu uzoefu wake, Regina Mohamedi alisema mbegu hizo zilimsaidia kupata mavuno ya kutosha kwa matumizi ya familia pamoja na ziada ya kuuza.
“Mvua zilipokatika nilidhani hatutavuna chochote, lakini mbegu hizi zilinipa matumaini mapya. Nimepata chakula cha familia na nimeuza kiasi kidogo, jambo ambalo limenisaidia kuongeza kipato,” alisema Regina.
Kwa upande wake, Sada Masoudi alisema mafanikio hayo yameongeza kujiamini na nafasi ya wanawake katika shughuli za kilimo.
“Sasa tunajivunia kilimo chetu. Mbegu zinazostahimili ukame zimetuwezesha wanawake kujitegemea na kuhakikisha familia zetu zinapata chakula hata wakati wa mvua chache,” alisema Sada.
Wanawake wakulima hao wanahamasisha wenzao kutumia mbegu za kisasa zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wakisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa kaya vijijini.
Kwa upande wa vijana, mbinu hizi zimeanza kubadilisha mtazamo wao kuhusu kilimo. Baadhi yao wameanza kuona kilimo kama fursa ya kiuchumi, wakitumia taarifa za hali ya hewa kufanya maamuzi ya kibiashara kuhusu muda wa kupanda na aina ya mbegu. Mafanikio haya yanaakisi mjadala wa COP30 unaosisitiza kuwa teknolojia rahisi na taarifa sahihi vinaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa jamii za vijijini.
Changamoto: Gharama, Taarifa na Usawa wa Kijinsia
Licha ya mafanikio hayo, msimu uliopita uliibua changamoto nyingi kwa wanawake na vijana wa Tabora, Changamoto kubwa ilikuwa upatikanaji na gharama ya mbegu bora. Wakulima wengi walilazimika kupanda kwa kuchelewa au kutumia mbegu za kienyeji kutokana na kukosa fedha, hali iliyopunguza mavuno yao.
Changamoto nyingine ilikuwa upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka. Wakulima walioko maeneo ya mbali walikosa kabisa taarifa au walipata utabiri usioeleweka vizuri, jambo lililosababisha maamuzi yasiyo sahihi ya kilimo. Hili linaakisi mjadala wa COP30 kuhusu pengo kati ya teknolojia zilizopo na uwezo wa jamii maskini kuzifikia.
Wanawake walikumbana zaidi na changamoto za umiliki wa ardhi na mamlaka ya maamuzi. Katika kaya nyingi, wanawake hawakuwa na sauti ya mwisho kuhusu aina ya mbegu au muda wa kupanda, hata pale walipopata taarifa sahihi za hali ya hewa. Hali hii ilipunguza uwezo wao wa kunufaika kikamilifu na teknolojia za kilimo himilivu cha tabianchi.
Kwa vijana, changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa mitaji na mikopo. Wengi wao hawakuwa na dhamana ya kupata mikopo ya pembejeo, hali iliyowafanya kulima kwa kiwango kidogo au kutumia mbinu zisizoendana na hali ya mabadiliko ya tabianchi. Changamoto hizi zimekuwa zikijadiliwa pia katika COP30, ambapo wito umetolewa kwa fedha za tabianchi kufika moja kwa moja kwa vijana na wanawake.
Mwelekeo wa Baadaye Katika Muktadha wa COP30
Uzoefu wa msimu uliopita umeonesha kuwa wanawake na vijana wa Tabora wana uwezo mkubwa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi endapo watapatiwa mbegu nafuu, taarifa sahihi na msaada wa kifedha. Haya ndiyo masuala makuu yanayosisitizwa katika COP30, hususan kuhusu haki ya usawa wa kijinsia, ushiriki wa vijana na ufadhili wa kukabiliana na tabianchi.
Wadau wa maendeleo, serikali na mashirika ya kijamii wanahimizwa kuimarisha mifumo ya usambazaji wa taarifa za hali ya hewa, kuongeza ruzuku ya mbegu bora na kuweka mifumo rafiki ya mikopo kwa vijana na wanawake. Hatua hizi zitasaidia kugeuza mjadala wa COP30 kuwa matokeo halisi mashambani.
Kwa ujumla, msimu uliopita wa kilimo Tabora umebainisha kwa uwazi kuwa mjadala wa COP30 si wa nadharia pekee. Mafanikio na changamoto za wanawake na vijana wanaotumia utabiri wa hali ya hewa na mbegu zinazohimili ukame ni ushahidi kuwa suluhisho la tabianchi linaanzia kwenye shamba la mkulima mdogo. Kilichobaki sasa ni kuhakikisha kuwa ahadi za kimataifa zinawafikia wale walio mstari wa mbele kuhimili athari za tabianchi kila siku.
Social Plugin