Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBINU ZA KILIMO CHA KUHIFADHI ARDHI ZINAIMARISHA USTAWI WA WAKULIMA NA KUPAMBANA NA MMOMONYOKO

 

Na Hadija Omary Mazezele.

Wakulima wa mkoa wa Tabora sasa wameanza kutumia mbinu za kilimo cha kuhifadhi ardhi ikiwa ni sehemu ya jitihada kubwa za kukabiliana na mmomonyoko wa udongo, kupunguza uharibifu wa ardhi na kuboresha tija ya kilimo, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame na mvua zisizo thabiti.

Kilimo cha kuhifadhi ardhi kinajumuisha matumizi ya mabaki ya mazao kama giligilani, maganda ya nafaka na mabaki mengine ya mimea kufunika udongo ili kulinda rutuba yake, kupunguza kuharibika kwa udongo kwa mvua za awali na kuruhusu unyevu kubaki shambani. 

Mbinu hii, pamoja na kilimo cha kuhifadhi (conservation agriculture) kama kupanda kwa mbinu ya doa (ripping), matumizi ya mbolea asili na mzunguko wa mazao  imeonekana kusaidia wakulima kupata mavuno bora hata wakati mvua haipatikani kwa wingi. 

Mbinu hizi zinaendana moja kwa moja na maazimio ya COP30 yanayohimiza kilimo himilivu cha tabianchi (climate-resilient agriculture) ili kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuzuia kupotea kwa rutuba na kuongeza uwezo wa mashamba kustahimili ukame na mvua zisizotabirika.

Wadau mbalimbali wa maendeleo wanashirikiana na wakulima katika mkoa wa Tabora kutekeleza mbinu hizi za kuhifadhi ardhi ambapo Moja ya mashirika hayo ni Caritas Tabora, shirika la kijamii ambalo limekuwa likisaidia jamii tangu 1976 kupitia miradi ya maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula na kuhimiza mbinu endelevu za uzalishaji. 

Ingawa shirika hili pia linashughulikia misaada ya dharura, limetumia uzoefu wake kuwajengea uwezo wakulima juu ya mbinu za kilimo endelevu zinazosaidia kuhifadhi udongo na mazingira kwa ujumla. 

Akieleza mchango wa Caritas Tabora, Afisa Kilimo na Mifugo wa shirika hilo, Melkizedeck Boniventure, alisema kuwa lengo kubwa ni kuwawezesha wakulima kujitegemea kupitia matumizi sahihi ya rasilimali walizonazo.

“Tunawasaidia wakulima kwa kuwajengea uwezo juu ya mbinu bora za kilimo na ufugaji endelevu zinazosaidia kuhifadhi rutuba ya udongo na kulinda mazingira. Hii inawafanya wakulima wawe na uzalishaji endelevu hata katika mazingira yenye changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Boniventure.

Aliongeza kuwa kupitia mafunzo ya vitendo, ufuatiliaji wa mashamba darasa na ushirikishwaji wa jamii, Caritas Tabora imefanikiwa kuongeza uelewa wa wakulima juu ya umuhimu wa uhifadhi wa ardhi na matumizi sahihi ya pembejeo.

“Hatufundishi tu nadharia, bali tunafanya kazi moja kwa moja na wakulima mashambani. Hii inasaidia kuhakikisha mbinu wanazofundishwa zinaeleweka na kutekelezwa kwa vitendo,” aliongeza.

Wakulima wa mkoa wa Tabora wameeleza kufurahishwa na ushirikiano huo, wakisema umechangia kuboresha uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuhifadhi mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kupitia mafunzo na ushauri wa kitaalamu uliotolewa na Caritas Tabora, Jumanne Mabula ambaye ni mkulima wa kata ya Ndevelwa Manispaa ya Tabora aliweza kujifunza mbinu bora za kilimo endelevu zinazolenga kuhifadhi rutuba ya udongo, kutumia pembejeo kwa usahihi na kuongeza uzalishaji.

Akizungumza kuhusu manufaa aliyoyapata, Jumanne alisema ushirikiano huo umebadilisha mtazamo wake juu ya kilimo.

“Kabla ya kushirikiana na Caritas Tabora, uzalishaji ulikuwa mdogo na udongo ulikuwa unachoka haraka. Kupitia mafunzo yao, nimejifunza mbinu za kuhifadhi ardhi na sasa mavuno yameongezeka huku mazingira yakilindwa,” alisema Jumanne.

Aliongeza kuwa matokeo hayo yamechangia kuimarika kwa usalama wa chakula katika familia yake na kuongeza kipato.

“Sasa familia yangu inapata chakula cha kutosha na ninauza ziada. Hii inanipa matumaini kuwa kilimo endelevu kinaweza kuboresha maisha yetu na ya vizazi vijavyo,” aliongeza.

Wakulima wa Tabora wanaamini kuwa ushirikiano na mashirika kama Caritas Tabora ni nguzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha maendeleo endelevu ya kilimo.

Hatua hizi zinaakisi wito wa COP30 unaosisitiza kuwa mashirika ya kijamii na ya kidini yana nafasi muhimu katika kufikisha ajenda ya tabianchi ngazi ya chini, ambako athari zake zinaonekana moja kwa moja.

Wakulima wa Tabora wanaeleza faida kadhaa za kutumia kilimo cha kuhifadhi ardhi ikiwemo Kupunguza mmomonyoko wa udongo Mabaki ya mazao yaliyowekwa juu ya ardhi huzuia ardhi kuuzwa na maji ya mvua na upepo, hivyo kuweka rutuba inapoendelea kuwa shambani.
Kuboresha unyevu wa udongo,Udongo wenye kiwango cha juu cha unyevu husaidia mimea kustawi, hasa wakati wa ukame au mvua za wastani duni.

Kuongeza rutuba na mavuno,Mbinu za kilimo mseto na kilimo endelevu huongeza virutubisho vya udongo, na hivyo kusaidia wakulima kupunguza utegemezi wa pembejeo ghali.
Kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, Kwa kutumia mbinu hizi, wakulima wanaweza kustawisha mashamba yao dhidi ya hali ngumu ya hewa kama ukame, mojawapo ya changamoto kuu kwa Tabora. 

Mabadiliko ya tabianchi, kama ukosefu wa mvua za kutosha na mifumo isiyotabirika ya mvua, yamekuwa changamoto kwa wakulima wa Tabora,Mbinu za kilimo cha kuhifadhi ardhi pamoja na kazi ya mashirika kama Caritas Tabora na taasisi za utafiti zimewatia wakulima nguvu mpya za kukabiliana na changamoto hizi kwani wanaweza kuongeza tija ya shamba lao huku wakilinda ardhi na mazingira kwa vizazi vijavyo.

Kwa ujumla, kilimo cha kuhifadhi ardhi kinachotekelezwa Tabora kwa kushirikiana na Caritas Tabora ni mfano hai wa jinsi mijadala ya kimataifa ya COP30 inavyoweza kutafsiriwa kuwa suluhisho la kweli mashambani. Ni ushahidi kuwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi hayaanzi kwenye mikutano ya kimataifa pekee, bali yanaanzia kwenye udongo unaolimwa na mkulima wa kawaida.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com