Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBEGU ZA MAZAO ZINAZOSTAHIMILI UKAME ZAANZA KUTUMIWA TABORA

Na Hadija Omary Mazezele

Wakati dunia ikiendelea kujadili athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Tabianchi COP30 ulioangazia kwa kina masuala ya kukabiliana na athari za tabianchi (adaptation), wakulima wa mkoa wa Tabora wameanza kushuhudia utekelezaji wa vitendo wa ajenda hiyo kupitia matumizi ya mbegu za mazao zinazostahimili ukame na zinazokomaa haraka, hususan mahindi na mpunga.

Katika mijadala ya COP30, nchi zinazoendelea zilisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kilimo himilivu cha tabianchi (climate-smart agriculture) kama njia ya kulinda usalama wa chakula kwa jamii zinazotegemea mvua,Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi na mabadiliko ya mifumo ya mvua, imeanza kutafsiri ajenda hiyo kwa vitendo kupitia utafiti na usambazaji wa mbegu bora.

Katika msimu huu wa kilimo, wakulima wa Tabora wanaonyesha shauku kubwa juu ya matumizi ya mbegu za mazao zinazostahimili ukame hasa mahindi na mpunga zinazokomaa haraka huku serikali na wadau wa kilimo wakifanya juhudi za kuhakikisha mbegu hizi zinapatikana kwa wakulima kwa wakati na kwa bei inayowezekana kuimudu.

Mbegu bora za mazao kama mahindi na mpunga zilizoboreshwa kwa sifa za kustahimili ukame, magonjwa na kutoa mavuno mengi zimeanzisha kutumika katika mfumo wa kilimo nchini Tanzania.

Kwa mfano, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) imebuni na kusambaza mbegu bora za mpunga kama TXD306 (SARO 5), SUPA BC, TARI RIC1 na RIC2 ambazo zinatengenezwa kukua hata kwa hali ya mvua duni na wakati wa msimu mfupi wa mvua, Pia zimetoa aina za mahindi kama CH1 na CH2 ambazo zinazo sifa za kustahimili mazingira magumu.

Mbegu nyingi zilizopo sasa zinakusudiwa hasa kwa maeneo yaliyo hatarini kwa ukame. Kwa mahindi, aina mbalimbali zimeboreshwa ili kustahimili kukauka na bado kutoa uzalishaji mzuri. Mbegu hizi zimefanyiwa utafiti na zinapatikana sokoni kupitia vituo vya usambazaji ya mbegu. Kwa upande wa mpunga, aina kama NERICA (New Rice for Africa) na mbegu nyingine za haraka kukomaa zinapatikana na hutumika kwa maeneo yenye mvua kidogo au msimu mfupi.

Upatikanaji wa mbegu za ubora unaendelea kuimarishwa kupitia serikali, mashirika ya kisera ya kilimo, na wazalishaji wa mbegu.

Taasisi za utafiti kama TARI na kampuni za mbegu zinaendelea kuzalisha na kuuza mbegu kwa wakulima kwa msimu huu. Mbegu hizi zinapatikana kupitia vituo vya usambazaji vya Wakala wa Mbegu na pia kwa wakulima kupitia soko la kawaida. Serikali pia ina mpango wa ruzuku ya mbegu za mahindi ili kuwasaidia wakulima kupata mbegu hizi kwa gharama nafuu ili kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula.

Wakulima wa Tabora wameripoti kwamba mbegu hizi zina uwezo wa kukua hata wakati mvua si nyingi na zinaweza kukomaa haraka ikilinganishwa na mbegu za zamani za kienyeji ambapo Hii inatoa matumaini ya mavuno bora zaidi licha ya mabadiliko ya hali ya hewa yanayoweza kuathiri msimu wa kilimo.

Wakulima wa kijiji cha Igombe  Manispaa ya Tabora wameanza kuona mwanga mpya wa mafanikio ya kilimo baada ya kuanza kutumia mbegu za kisasa zinazostahimili ukame na kukomaa kwa haraka. 

Miongoni mwa wakulima wanaonufaika na mbegu hizo ni Juma Mohamedi na Rehema Mihambo, ambao wanasema mabadiliko hayo yameleta matumaini makubwa licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima hao wameripoti kuwa mbegu wanazotumia zina uwezo wa kukua hata wakati mvua inapokuwa chache, tofauti na mbegu za zamani za kienyeji ambazo zilihitaji mvua nyingi na muda mrefu zaidi wa kukomaa.

Akizungumza kuhusu uzoefu wake, Juma Mohamedi alisema matumizi ya mbegu za kisasa yamepunguza hofu aliyokuwa nayo kila msimu wa kilimo.

“Zamani tulikuwa tunaomba mvua isinyeshe kidogo wala isichelewe, lakini sasa hata mvua ikipungua bado mazao yanastawi. Mbegu hizi zimetupa ujasiri na matumaini mapya,” alisema Juma.

Kwa upande wake, Rehema Mihambo alisema mbegu hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji na kumsaidia kujipanga kiuchumi.

“Mbegu za kisasa zimenirahisishia kazi. Zinakomaa mapema na mazao yanakuwa mazuri. Ninaamini hata familia yangu itanufaika zaidi kupitia mavuno haya,” alisema Rehema.

Wakulima wa Igombe wanaamini kuwa matumizi ya mbegu za kisasa ni suluhisho muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, huku wakihamasisha wakulima wengine kuachana na mbegu za zamani na kukumbatia teknolojia ya kisasa ya kilimo kwa maendeleo endelevu

Aidha Mbegu za mazao zinazostahimili ukame, kama mahindi na mpunga zinazokomaa haraka, zinapatikana sasa kwa wakulima Tabora kupitia vituo rasmi na usambazaji wa mbegu za bodi. Bei bado ni changamoto kwa wakulima wadogo, lakini mpango wa ruzuku na upatikanaji kupitia vikundi unaweza kusaidia wakulima wengi kupata mbegu hizi kwa bei nafuu.

Matumizi ya mbegu za mazao zinazostahimili ukame Tabora ni mfano halisi wa jinsi maamuzi na mijadala ya kimataifa kama COP30 yanavyoweza kutafsiriwa kuwa hatua za moja kwa moja kwa wakulima. Hata hivyo, ili ajenda hiyo iwe na matokeo ya kudumu, kunahitajika kuimarishwa kwa ruzuku, upatikanaji wa fedha za tabianchi na elimu kwa wakulima ili teknolojia hizi ziweze kufikiwa na wengi zaidi.

Mbinu za Kilimo cha Kuhifadhi Ardhi Zinaimarisha Ustawi wa Wakulima na Kupambana na Mmomonyoko

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com